G20 kupendekeza ushirikiano na Afrika
2 Juni 2017Mkutano huo utakaoandaliwa Berlin, Ujerumani utakua kuhusiana na ahadi za Ujerumani wakati wa urais wake wa G20, ambapo ilisema itatafuta mbinu za kufanya kazi pamoja baina ya nchi zilizoendelea kiviwanda na nchi zinazoendelea na hata bara Afrika, ili kupunguza umasikini katika bara hilo.
Mwaka jana Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliahidi na nikiyanukuu maneno yake, "Pamoja na misaada ya maendeleo, tutashughulika na kuhakikisha kuwa tunapata njia nzuri za kupigia debe maendeleo ya kiuchumi Afrika," mwisho wa kunukuu.
Katika mkutano huo, G20 inataka kuonesha kwamba inayatimiza yale yaliyoko katika mpango wake wa "Mshikamano na Afrika", ambapo mpango huo wa serikali ya Ujerumani unalenga kuhakikisha kwamba uwekezaji zaidi wa kibinafsi unaelekea Afrika na suala la ukosefu wa ajira likabiliwe.
Nchi tano za Afrika tayari zinashiriki mpango huo
Ludger Schuknecht ni Mchumi Mkuu katika wizara ya fedha ya Ujerumani na anasema, "suala jipya ni kwamba washirika muhimu ambayo ni mataifa ya Afrika, mashirika ya kimataifa na nchi zengine yanafanya kazi pamoja."
Nchi tano za Afrika tayari zinashiriki mpango huo nchi hizo zikiwa Ivory Coast, Morocco, Rwanda, Senegal na Tunisia huku nchi nyengine zikitarajiwa kujiunga na mpango huo baadae. Mbali na mataifa ya G20, Shirika la Fedha Duniani IMF, Benki ya Dunia na ile Benki ya African Development wanashiriki katika mpango huo wa "Mshikamano na Afrika."
Umuhimu wa mpango huo ni ushirikiano wa uwekezaji ambapo nchi za Afrika zimejitolea kufanya mabadiliko ili kuwavutia wawekezaji na mashirika ya kimataifa pamoja na nchi washirika, zinawapa usaidizi wa kiufundi na kifedha. Fauka ya hayo, mataifa ya G20 yanataka kuzitia motisha kampuni zilizo katika nchi zao kuwekeza zaidi Afrika.
Kwa sasa wawekezaji wengi wamesusia kuwekeza Afrika kutokana na ufisadi wa kiwango cha juu katika nchi za bara hilo na ukosefu wa ustawi wa kisiasa. Mwaka 2016, uwekezaji wa moja kwa moja Afrika, ulifikia Dola bilioni 51 za Kimarekani, hicho kikiwa ni kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na mabara mengine, na suali ni je mpango huo wa "Mshikamano na Afrika" utalibadili hilo?
Nchi maskini zaidi zinastahili kujumuishwa pia katika mpango huo wa "Mshikamano na Afrika"
Jörg Wellmeyer ni Mkurugenzi Mkuu katika shirika la kimataifa la Strabag na katika mahojiano na DW, alisema, "ni mpango mzuri na unatoa suluhu kwa matatizo mengi. Kampuni zinaweza kuzalisha bidhaa za soko la Afrika, barani Afrika. Kuuza kutoka bara lengine ni ghali mno."
Lakini katika nchi nyingi za Afrika, hakuna wateja wa kutosha wa bidhaa hizo, kwa hiyo, vikwazo vya ushuru ni sharti vivunjwe ili bidhaa hizo zipate kuuzwa katika kila eneo la Afrika. Lakini Wellmeyer alisema "hili ni jambo litakalochukua muda wa kuanzia miaka mitano au zaidi."
Stephan Exo-Kreischer kutoka shirika la sera za maendeleo alisema sio tu zile nchi zilizokwishastawi kimaendeleo ndizo zinazostahili kuangaziwa, bali zile nchi dhaifu na masikini zaidi zinastahili kujumuishwa katika mpango huu."
Mwandishi: Daniel Pelz/DW HA Afrika
Tafsiri: Jacob Safari
Mhariri: Mohammed Khelef