1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gambia yasitisha adhabu ya kifo

19 Februari 2018

Rais wa Gambia Adama Barrow ametangaza kusitisha adhabu ya kifo katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika wakati ikiwa kwenye juhudi za kutambulika tena kimataifa baada ya kuondolewa kwa Rais wa zamani Yahya Jammeh.

https://p.dw.com/p/2svv2
Gambia Präsident Adama Barrow
Rais wa Gambia Adama BarrowPicha: DW

 Rais wa Gambia Adama Barrow ametangaza kusitisha adhabu ya kifo katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika wakati ikiwa kwenye juhudi za kutambulika tena kimataifa baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa mtawala wa muda mrefu nchini humo Yahya Jammeh.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty international, utekelezwaji wa adhabu ya kifo unaendelea kushuka barani Afrika ambapo serikali katika bara hilo ziIitekeleza adhabu hiyo kwa watu 22 mwaka 2016 ikilinganishwa na watu 43 mwaka 2015.

"Nitatumia nafasi hii kutangaza kusitishwa kwa adhabu ya kifo Gambia ikiwa ni hatua ya mwanzo kuiondoa," Alisema Rais huyo wa Gambia katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya miaka 53 tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Waingereza.

Ushindi dhidi ya udikteta

Rais Barrow Amesema kuwa nchi hiyo imeshinda vita dhidi ya udikteta jambo ambalo ni jepesi kuliko changamoto kubwa ya kuendeleza amani ili kukuza demokrasia nchini humo. "Makosa yatatokea lakini tutayarekebisha kwa kadri tunavyofanya kazi ya kuijenga Gambia mpya," aliongeza Barrow.

Kiongozi wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh aliyeikimbia nchi hiyo mwaka mmoja uliopita baada ya kushindwa kuchaguliwa tena katika uchaguzi alikosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa mwaka 2012 baada ya serikali yake kuwaua ghafla wafungwa tisa kwa kuwapiga risasi.

Rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa zamani wa Gambia Yahya JammehPicha: Reuters/T. Gouegnon

Tamko la Rais wa sasa wa Gambia ambaye kabla ya kushika wadhifa huo aliwahi kufanya kazi kama mlinzi huko London Uingereza, limekuja ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kutia saini makubaliano kati ya serikali yake na umoja wa mataifa.

Tangu aingie madarakani mwaka mmoja uliopita Rais Barrow, amejaribu kuirejesha katika mstari Gambia ambayo sifa yake ilichafuliwa na utawala wa Jammeh kwa miaka 23, utawala uliokuwa umegubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo, kukamatwa kiholela, raia kutoweka, mauaji, pamoja na migongano na nchi za kigeni.

Serikali ya Barrow yenye mwaka mmoja tangu iingie madarakani imeanza kufanya mabadiliko ya mfumo wa mahakama na katiba huku bunge la nchi hiyo likiwa katika hatua ya kutunga sheria ili kuanzisha tume ya ukweli, maridhiano na fidia pamoja na tume ya haki za binadamu.

Mapema mwezi huu Gambia ilijiunga tena na nchi zinazounda jumuiya ya Madola, Common Wealth, ambayo Jammeh alijitoa tangu mwaka 2013 na kuiita jumuiya hiyo kuwa ni taasisi ya ukoloni mamboleo.

Mwandishi: Angela Mdungu /AP/RTE/AFPE

Mhariri: Joseph Charo.