1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gauck awataka Wajerumani kuwasaidia wakimbizi

Abdu Said Mtullya24 Desemba 2014

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani amewataka raia wa nchi hiyo kuonesha huruma, ukarimu na upole kwa wakimbizi, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake wa Krismasi kwa taifa.

https://p.dw.com/p/1E9dN
Bundespräsident Joachim Gauck Weihnachtsansprache
Picha: picture-alliance/dpa/M. Sohn

Rais Gauck amewataka wananchi wa Ujerumani wawe tayari kusaidia badala ya kujifungia ndani ya mipaka yao na kujitenga na wengine. Bwana Gauck ameitaka Ujerumani iwe jamii ya uwazi.

Amesema pale ambapo Ujerumani inaweza kutoa mchango katika kudumisha amani na kusaidia katika juhudi za kupunguza dhiki , itapasa kufanya kila linalolazimu.

Juu ya kuwa tayari kuonyesha huruma kwa wakimbizi Rais wa Ujerumani amesema Wajerumani watakuwa na furaha na faraja ikiwa watawashirikisha wengine katika kile ambacho wao wenyewe wanatumai kukipata.

Rais wa shirikisho la Ujerumani amewapongeza wananchi wake kwa kujitokeza kwa wingi kupinga tabia ya kujifungia ndani ya mipaka yao na kujitenga na wengine.Gauck amesema kuwa mtazamo huo umempa moyo .

Katika ujumbe wake wa Krismasi ,Gauck pia amewaambia wananchi wa Ujerumani kwamba hawana haja ya kuwa na hofu juu ya dunia inayowazunguka. Badala yake amewashauri wananchi wake wajaribu kuzielewa changamoto zinazoikaili jamii yao na pia wayazingatie maadili yao.

Maandamano dhidi ya Uislamu mjini Dresden, maarufu kama PEGIDA.
Maandamano dhidi ya Uislamu mjini Dresden, maarufu kama PEGIDA.Picha: picture-alliance/dpa/Hendrik Schmidt

Bwana Gauck aliekuwa mchungaji wa Kiprotestanti na mtetezi wa haki za kiraia katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki, ametilia maanani katika hotuba yake kwamba watu wengi wana wasi wasi kutokana na vita na vitendo vya ugaidi ambavyo amesema vinafanyika kwa kulitumia jina la dini.

Mwaka wa migogoro na vita

Rais wa Ujerumani ameeleza kwamba wakati mwaka huu unapoagwa inapasa kukumbuka yaliyotokea katika mwaka huo. Amesema mwaka huu ulikuwa wa migogoro, vita ,mauaji na ugaidi uliofanywa kwa kulitumia jina la dini.Amesema Kila siku watu wanauliwa.

Katika ujumbe wake wa Krismasi Rais wa Ujerurmani pia amewapongeza Wajerumani wanaoshiriki katika harakati za kupambana na maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika magharibi. Pia amewapongeza askari wa Ujerumani wanaoshiriki katika juhudi za kuleta amani katika sehemu mbalimbali za dunia.

Waomba hifadhi nchini Ujerumani na waungaji mkono wao wakibeba mabango ya kushajiisha kukubaliwa kwa wakimbizi.
Waomba hifadhi nchini Ujerumani na waungaji mkono wao wakibeba mabango ya kushajiisha kukubaliwa kwa wakimbizi.Picha: Getty Images/Patrick Lux

Bwana Gauck ameelezea matumaini kwamba masuluhisho yanaweza kupatikana. Amesema japo siyo rahisi kuyaleta masuluhisho hayo,litakuwa jambo la kukatisha tamaa ikiwa watu watakuwa na hofu.

Bila ya kutumia kauli ya uwazi Rais Gauck amezungumzia juu ya jumuiya ya watu wanaojiita " Pegida." katika miezi ya hivi karibuni Ujerumani imeshuhudia kuibuka wimbi la maalfu ya watu wanaoandamana kuupinga Uislamu katika miji kadhaa .

Wazalendo wanaoupinga Uislamu barani Ulaya

Watu hao wanajiita wazalendo waopinga kusilimishwa kwa magharibi, Watu hao wanafanya maandamano kila wiki. Jumatatu iliyopita watu 17,500 walishiriki katika maandamano kama hayo.Lakini wakati huo huo wananchi wengine wa Ujerumani pia wamekuwa wanajitokeza kuwapinga watu hao.

Mwandishi: Mtullya Abdu
Mhariri: Mohammed Khelef