Gaza. Abbas kuivunja serikali ya Palestina?
20 Oktoba 2006Waziri mkuu wa Palestina Ismail Haniyeh wa chama cha Hamas amesema leo kuwa atakataa hatua zozote za rais Mahmoud Abbas za kuiondoa serikali yake, akionya kuwa juhudi kama hizo hazitapunguza hali ya wasi wasi ambayo imeleta hali ya kitisho cha kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Haniyeh amesema kuwa haitakuwa na maana kwa Abbas kuivunja serikali, akidokeza kuwa utawala wowote wa muda utakaoteuliwa na rais hautapata kuidhinishwa na bunge, ambalo linadhibitiwa kwa wingi mkubwa na chama cha Hamas.
Abbas ametoa ishara kuwa anaweza kuivunja serikali inayoongozwa na chama cha Hamas baada ya juhudi za kuunda baraza la mawaziri la umoja wa kitaifa kushindwa kutokana na Hamas kukataa kulegeza msimamo wao kuhusu Israel.