GAZA:Mapigano kati ya Israel na Palestina yaendelea
22 Mei 2007Israel na wapiganaji wa kipalestina wamendelea kurushiana makombora, katika siku ya tatu ya mapigano kati ya pande hizo.
Wapalestina watano na mwanamke mmoja wa Kiisrael wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni.
Mwanamke huyo aliuawa baada ya roketi kurushwa na kuangukia gari lake katika mji wa kusini mwa Israel wa Sderot, ikiwa ni mara ya kwanza kwa makombora ya kipalestina kusababisha madhara kwa Israel toka mwezi Novemba mwaka jana.
Mapema hapo jana Israel ilifanya mashambulizi makali ya anga na kuwaua wapiganaji wanne wa kundi la Jihad.
Baraza la Usalama la Israel lilikubaliana hapo siku ya Jumapili kuendelea na mashambulizi dhidi ya Palestina ikiwa ni katika kujibu mashambulizi ya makombora kiasi cha 150 yaliyovurumishwa kutoka Gaza toka wiki iliyopita.
Waziri wa miundo mbinu ya kitaifa wa Israel Binyiman Ben-Eliezer amesema kuwa ni lazima wawaangamize viongozi wa wanamgambo hao wa kiislam.