1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gesi ya sumu yauwa 7 Kongo baada ya volkano kuripuka

25 Mei 2021

Siku chache baada ya mripuko wa volkano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kiwango cha gesi hatari kimeendelea kuongezeka katika baadhi ya maeneo ambako tope la moto la volkano hiyo bado linachemka.

https://p.dw.com/p/3tuji
Weltspiegel | Goma, Kongo | Vulkanausbruch
Picha: Justin Kakumba/AP/dpa/picture alliance

Wakati huu ambapo shughuli zimeanza kurejea upya mjini Goma kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la gesi inayotishia maisha ya wananchi ambao wamepakana na maeneo yaliyofunikwa na tope la volkano.

Siku ya Jumatatu (Mei 24), miili ya watu saba ilikutwa katika kijiji cha Kibati mbali kidogo na mji wa Goma, ambapo vyanzo vilieleza watu hao walikuwa wakijaribu kuvuuka tope la moto kutoka kwenye volkano hiyo na kufariki kutokana na gesi.

Mkuu wa Taasisi ya Uchunguzi wa Milima ya Moto, Kasereka Mahinda, alithibitisha vifo hivyo akisema kuwa hali ilikuwa bado ni mbaya zaidi.

Hadi siku ya Jumanne (25 Mei), wananchi walioathirika na mripuko huo wa volkano walikuwa bado hawajapatiwa msaada wowote, huku wengi wao wakiwa wamehifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Bado hakuna msaada kwa waathirika

Kongo Goma Mount Nyiragongo Vulkanausbruch  Lava
Matope ya mripuko wa volkano ya Mlima Nyiragongo, Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: Justin Katumwa/AFP/Getty Images

Mji wa Goma uliripotiwa kushuhudia uhaba mkubwa wa vyakula na kuonekana kuwa kitisho kwa maelfu ya wakaazi walioyakimbia makaazi yao wakati wa mripuko. 

Kiongozi wa ujumbe wa mawaziri kutoka Kinshasa, Mbunga Jean Jacque, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa juhudi zimeanzishwa ili kuwasaidia waathirika wa janga hilo.

Mbali ya tope hilo la moto kutoka kwenye volkano iliyoishia katika kijiji cha Buhene viunga vya mji wa Goma, Mlima Nyiragongo ulikuwa ukiendelea kutoa moshi pamoja na majivu ambayo kulingana na wataalamu wa milima ya moto ni gesi inayoweza kuhatarisha maisha ya wananchi wanaoishi kando mwa eneo hilo. 

Wakaazi wa huko waliripoti kuwa mipasuko ya ardhi imeanza kuonekana katika baadhi ya maeneo mjini Goma, hali iliyowatia wasiwasi katika wakati ambapo bado mitetemeko midogo midogo ya ardhi ilikuwa ikiendelea kuutikisa mji huo.

Ripoti imeandikwa na Benjamin Kassembe, DW Goma