Ghasia zaendelea Misri,watu kadhaa wauawa
6 Julai 2013Rais huyo wa kipindi cha mpito ameichukua hatua hiyo wakati wafuasi wa Rais alieangushwa, Mohammed Mursi na wanaompinga, wameendelea kupambana katika mitaa ya miji ya Cairo, Alexandria na kwingineko.
Maalfu kwa maalfu ya wafuasi wa Mursi wanataka mwanasiasa huyo aliechaguliwa kwa njia za kidemokrasia arudishwe madarakani. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari watu wapatao 30 wameshauwawa hadi sasa nchini Misri.
Ghasia hizo zinafuatia hatua ya jeshi la Misri mapema wiki hii ya kumwondoa madarakani Mohammed Mursi.Ghasia zilianza jana mchana wakati wafuasi wa Mursi walipoandamana na kwenda kwenye makao makuu ya jeshi mjini Cairo na kuwafanya askari wanaoyalinda makao makuu hayo wafyatue risasi.
Ilipoingia jioni kundi la wafuasi wa Mursi liliandamana kupitia kwenye daraja la"October "kwenye mto wa Nile na kuwashambulia wapinzani wa Mursi waliokusanyika karibu na uwanja wa Tahrir,na nje ya makao makuu ya Televisheni ya serikali.
Mahasimu hao walipambana kwa muda wa saa kadhaa.Waislamu wenye itikadi kali waliokuwa wamevaa kofia za chuma walikuwa na ngao za mabati za kujitengenezea wenyewe.
Pande mbili hizo zilishambuliana kwa mawe.
Shirika la habari la AP limeripoti kwamba milio ya risasi pia ilisikika.
Moto ulizuka kutokea kwenye gari iliyopigwa moto juu ya sehemu ya kutokea kwenye daraja. Huku mapambano yakindelea baina ya wanaomuunga mkono Mursi na wanaompinga, magari ya chuma ya jeshi la Misri yalikuwa yakipipita kwenye daraja na kuwatimua watu wanaomuunga mkono Mursi.
Mfungamano wa makundi ya Waislamu wenye itikadi kali,ikiwa pamoja na chama cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu yamepania kuendelea na maandamano ya amani. Wawakilishi wa Mfungamano huo wamesema umma wa Misri utaendelea kufanya maandamano ya amani kwa kukaa chini katika mji wa Cairo, hadi wanajeshi wayarudishe mamlaka na hadi Rais wa halali arudishwe madarakani.
Viongozi wa Udugu wa Kiislamu watiwa ndani:
Polisi wamewatia ndani maafisa waandamizi kadhaa wa chama cha Udugu wa kiislamu ikiwa pamoja na Khairat al-Shater anaezingatiwa kuwa mtu mwenye mamlaka makubwa baada ya Mohammed Mursi katika chama cha Udugu wa Kiislamu. Na kwa mujibu wa taarifa, polisi wanaendelea kuwakamata wanachama wa chama hicho.
Juu ya matukio ya nchini Misri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekakaririwa na msemaji wake akitoa mwito wa kuutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo. Amezitaka pande zote ziepuke kuchukua hatua za kulipiza kisasi. Katibu Mkuu Ban pia ametoa mwito wa kuzishirikisha pande zote katika mchakato wa kisiasa nchini Misri.
Mwandishi:Mtullya Abdu/afp,rtre
Mhariri: Amina Abubakar