1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghouta Mashariki yaendelea kushambuliwa

7 Machi 2018

Licha ya kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwalinda raia kwenye eneo la Ghouta Mashariki kwa kusitisha mapigano, taarifa zinaonesha kuwa mashambulizi yanaendelea kama kawaida.

https://p.dw.com/p/2tsYL
Syria Krieg
Picha: picture-alliance/Photoshot/A. Safarjalani

Mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, Zaid Ra'ad al-Hussein, amesema kuwa mzozo wa Syria sasa unaingia kwenye awamu mpya ya kuogofya zaidi, kukiwa na umwagaji damu mkubwa na wa makusudi huko Ghoutta Mashariki na ghasia zikizidi kwenye jimbo la Idlib, hali ambayo inawaweka watu milioni mbili kwqenye hatari. 

Kwa mujibu wa al-Hussein, kwa hali ilivyofikia sasa, ni lazima mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, iingilie kati rasmi na kuanzisha uchunguzi utakaopelekea kuwapandisha kizimbani wahusika:

"Lazima nisisitize kwamba tunachokiona Ghouta Mashariki na kwengineko Syria kinafanana na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Raia wanashambuliwa ili wajisalimishe au wauwawe. Watendaji wa uhalifu huu wanapaswa kujuwa kwamba wanatambulika, kwamba kesi zao zinakusanywa na kwamba watawajibishwa kwa wanayoyatenda. Syria lazima ipelekwe Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Jitihada za kuipuuzia haki na kuwalinda wahalifu ni jambo la aibu," alisema al-Hussein.

Kwa upande mwengine, mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria ameiomba serikali kuyaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye eneo la Ghouta Mashariki ili kuuruhusu msafara wa magari yenye madawa kufika huko.

Ali al-Za'taru amemuandikia barua Waziri wa Nje wa Syria, Faisal Mekdad, akimueleza kuwa katika msafara uliofikishwa huko Jumatatu, vifaa vyote vya matibabu vilishikiliwa na majeshi ya serikali badala ya kuruhusu kufikishiwa raia. Na hata baada ya kufika kwenye eneo husika, wafanyakazi wa misaada walishindwa kushusha mizigo iliyokuwemo, kutokana na vikosi vya serikali kuendelea kushambulia.

Mashambulizi yaendelea

Wakaazi wa Douma wakisaidiwa kutoka kwenye vifusi vya majengo baada ya mashambulizi ya anga ya jeshi la Syria.
Wakaazi wa Douma wakisaidiwa kutoka kwenye vifusi vya majengo baada ya mashambulizi ya anga ya jeshi la Syria.Picha: Reuters/B. Khabieh

Hayo yanakuja huku vikosi vya serikali vikiripotiwa kuendelea na mashambulizi yake ya angani, katika jitihada za kuligawa eneo linaloshikiliwa na waasi sehemu mbili. Picha za leo za matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni ya Syria zinaonesha viunga vya Mesraba vikitanda moshi, huku milio ya miripuko na ndege za kivita ikisikika.

Mtangazaji wa televisheni hiyo ya serikali alisema kuwa maeneo ya waasi yalikuwa yakilainishwa kwa mashambulizi ya anga, kabla ya kikosi cha ardhini kuchukuwa nafasi yake muda mfupi ujao. Khalil Aybour, mwanachama wa baraza la upinzani huko Ghouta Mashariki, amesema kuwa Mesraba inashambuliwa vikali leo.

Endapo vikosi vya serikali vitafanikiwa kukitia mikononi kiunga hicho, basi itakuwa hatua kubwa kuelekea nusu ya eneo la kaskazini mwa Ghouta, ukiwemo mji mkubwa kabisa wa Douma, kutokea upande wa kusini. 

Hadi sasa, vikosi hivyo vinashikilia zaidi ya asilimia 40 ya eneo hilo lililo karibu na mji mkuu, Damascus. Mashambulizi ya jeshi yalianza zaidi ya wiki mbili sasa, na yanatajwa kuwa moja ya operesheni za kikatili kabisa kuwahi kutekelezwa na utawala wa Rais Bashar Al Assad kwenye vita hivi vinavyoingia mwaka wake wa nane sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf