1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gianni Infantino ziarani Amerika Kusini

1 Aprili 2016

Rais wa Shirikisho la Kandanda la Kimataifa – FIFA Gianni Infantino yuko nchini Colombia katika mkondo wa nne wa ziara yake ya Amerika Kusini

https://p.dw.com/p/1IOE7
Paraguay Fifa PK Alejandro Dominguez & Gianni Infantino
Picha: picture-alliance/dpa/A.C. Benitez

Na mara tu baada ya kuwasili alikabiliwa na maswali kuhusiana na ripoti ya kutisha ya Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International kuhusu kutumikisha wafanyakazi katika ujenzi wa viwanja vya mpira kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar. Na Infantino alianza kwa kusema kuwa FIFA “haihitaji kuuokoa ulimwengu. Hiyo ni kazi ya mtu mwengine kufanya”. Alipoulizwa maswali zaidi, Infantino alisema "Zipo kazi nyingi ya kufanya lakini upo mchakato na, bila shaka FIFA ipo huko. Bila shaka FIFA imezungumza na maafisa nchini Qatar. Bila shaka FIFA inaiona hali hii na nadhani kuwa lazima sote tushirikiane katika kuimarisha hali ambayo haiwezi kufanywa kutoka siku moja hadi nyingine. Hilo ni wazi. Lakini nadhani hatua zimepigwa na nina uhakika kuwa mengi yatafanywa lakini FIFA itayafuatilia hayo yote".

Amnesty International inasema wafanyikazi katika uwanja wa Khalifa utakaoandaa mchuano wa ufunzi wa dimba la dunia wanalazimishwa kuishi katika mazingira machafu, wanalipa fedha nyingi ili kuajiriwa huku baadhi ya mishahara yao ikizuiliwa na kupokonywa pasipoti zao.

Infantino pia amesema kuwa FIFA itaiendeleza “sera ya kutovumilia rushwa” katika kandanda, ijapokuwa amesema hana mbinu ya muujiza katika kusuluhisha hilo. "Lazima tuwe wazi kabisa na kama mtu anataka kulitumia vibaya kandanda kwa maslahi yao ya kibinafsi ni vyema waondoke. Tunawapa uwezekano wa kuondoka kwa sababu la sivyo tutawatupa nje. Tuna sera mahsusi isoyovumilia kamwe masuala haya. Wanaotaka kutumia kandanda kwa maslahi yao wenyewe hawana nia nje kwa kandanda na hawapaswi kuwa katika kandanda".

Qatar imesema ina wasiwasi kuhusu madai hayo na kwamba itayachunguza. Serikali ilisema maslahi ya wafanyikazi wahamiaji yanapewa kipaumbele na kusisitiza kuhusu marekebisho ya sheria za kazi nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef