1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Girona yachupa kileleni La Liga baada ya kuifunga Barcelona

11 Desemba 2023

Klabu ya Girona imejiweka katika nafasi nzuri ya kuwania taji la ligi kuu ya Uhispania La Liga msimu huu baada ya kuilaza miamba wa Catalunya Barcelona mabao 4-2 na kuipiku Real Madrid kileleni mwa ligi.

https://p.dw.com/p/4a1fA
Mechi ya ligi kuu Uhispani kati ya FC Girona na Real Madrid
Wachezaji wa Girona wakisherehekea bao katika pambano dhidi ya Real MadridPicha: Joan Monfort/AP Photo/picture alliance

Mshambuliaji wa Ukraine Arten Dovbyk na Viktor Tsygankov walishirikiana kwa bao la kwanza la Girona huku Miguel Gutierrez, Valery Fernandez na Cristhian Stuani wakifunga bao kila mmoja na kupiga muhuri ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Uhispania.

Robert Lewandowski na Ilkay Gundogan waliifungia Barcelona mabao yao.

Mara baada ya ushindi huo, Kocha wa Girona Míchel Sánchez ameeleza furaha yake, "Sijui kama tunaweza kufikia kiwango cha Barcelona, Real Madrid na Atletico Madrid kwa msimu uliosalia. Hata hivyo, kiwango cha uchezaji kinaridhisha. Hawa wachezaji wanaweka historia na hicho ndicho kinachonipa furaha kwa sababu nadhani kila shabiki wa soka anaiunga mkono Girona, japo kwa kiasi."

Soma pia: Felix aiangamiza klabu yake ya Atletico Madrid

Uhispania | Kandanda | La Liga | FC Barcelona vs Valladolid CF
Mshambuliaji wa Barcelona Robert Lewandowski Picha: Joan Monfort/AP Photo/picture alliance

Ushindi huo wa kishindo, uliipaisha Girona hadi kileleni mwa La Liga ikiwa na alama 41, alama mbili mbele ya miamba Real Madrid yenye alama 39. Vijana wa Carlo Ancelloti walitoka sare ya 1-1 na Real Betis siku ya Jumapili.

Kwa sasa, Barcelona imeshuka hadi nafasi ya nne, ikiwa na alama 34 sawa na Athletico Madrid, yenye mechi moja mkononi. Mara ya mwisho kwa Barcelona kufungwa msimu huu ndani ya La Liga ilikuwa mwishoni mwa mwezi Oktoba dhidi ya Real Madrid.

Soma pia: Vinicius Jr. abaguliwa tena Uhispania

Kabla ya mechi ya jana, Barcelona ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo wowote katika mechi sita za hivi karibuni walizocheza dhidi ya Girona, huku wakipata ushindi mara nne na kutoka sare mechi mbili.

Barcelona ambayo itasafiri mnamo siku ya Jumatano kuelekea Ubelgiji kucheza dhidi ya Royal Antwerp katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, itacheza tena siku ya Jumamosi na Valencia katika ligi kuu ya Uhispania huku Girona ikiialika Alaves mnamo Disemba 18.