Gladbach wakamata usukani wa Bundesliga
28 Oktoba 2019Ushindi huo unawapa pointi 19 moja mbele ya mabingwa Bayern Munich, wakati Frankfurt wamerudi katika nafasi ya tisa. Marco Rose ni kocha wa Gladbach. "Ni vizuri kwa timu kwamba tuliweza kuhimili mikiki wakati wa kipindi kigumu. mechi hii ilikaribia kuharibika. lakini katika kipindi cha pili bila shaka ikawa nzuri kwetu - ijapokuwa nadhani hatukuwaruhusu hadi tukapata mabao yetu."
Awali, maamuzi yaliyotokana na VAR yaliigharimu Wolfsburg nafasi ya kwenda kileleni mwa ligi baada ya bao la dakika ya 84 la Joao Victor kufutwa katika sare tasa dhidi ya Augsburg. Refarii alilibatilisha kwa sababu lilikuwa la kuotea. Msikilize Maximilian Arnold, mchezaji wa VfL Wolfsburg. "Nadhani Augsburg walikuwa na mchezo mzuri sana. Walikuwa imara katika ulinzi. ilikuwa vigumu kwetu kupenya. kwa kweli, tulicheza vibaya leo. kwa hiyo ikawa vigumu sana. Lakini licha ya hayo, tulikuwa na nafasi moja, mbili, tatu katika kipindi cha kwanza na kama tungezitumia, nadhani tungeweza kuibuka washindi."
Wolfsburg sasa wanakamata nafasi ya nne na pointi 17 sawa na Freiburg. Ndio timu pekee katika ligi ambayo haijapoteza mechi.
Robert Lewandowski ndiye mchezaji wa kwanza wa Bundesliga kufunga bao katika kila mechi kati ya tisa za kwanza za msimu wakati Bayern ukiifunga Union Berlin 2 – 1 Jumamosi. Lewandowski aliichana rekodi iliyowekwa na Pierre-Emerick Aubameyang aliyekuwa amefunga katika mechi nane za kwanza katika msimu wa 2015 – 16.
Mpoland huyo sasa ana mabao 19 katika mechi 13 za Bayern kwenye mashindano yote. Hata hivyo ushindi huo mwembamba bado unazusha maswali kuhusu uwezo wa kocha Niko Kovac. Msikilize Thomas Muller. "Haukuwa mchezo rahisi kwa sababu hatukufaulu kuzitumia vyema nafasi tulizopata hasa katika umaliziaji langoni. Vinginevyo tulikuwa tumeonyesha mbinu nzuri. kwa mtazamo wangu, ilikuwa ni mechi tu nzuri kwetu kujaribu kuendeleza matokeo na kurejesha utulivu."
Na katika mtanange wa wikiendi wa derby ya 95 ya bonde la Ruhr ya watani wa jadi, wenyeji Schalke walitoka sare tasa na Borussia Dortmund. Schalke ambao wameimarika sana msimu huu chini ya kocha mpya David Wagner walipata nafasi nyingi za wazi lakini wakashindwa kuzitumia. Msikilize kocha Wagner. "Nadhani kutokana na matokeo ya leo unaweza kusema tulikuwa na nafasi kubwa na nzuri za kufunga bao. Kama kuna timu iliyostahili kushinda mechi hii, basi ni sisi. Katika ndondi, unaweza kusema tulishinda kwa pointi, lakini bahati mbaya hilo halifanyiki katika kandanda. Tulicheza mechi nzuri sana leo na nnajivunia vijana wangu na walichokifanya leo, katika debi dhidi ya Borussia Dortmund ilipendeza zaidi."
Freiburg waliwabwaga RB Leipzig 2 – 1. Bayer Leverkusen ilijiunga na Leipzig na Schalke katika pointi 15 kila mmoja baada ya kukosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya tatu, wakati ilipotoka sare ya 2 – 2 na Werder Bremen.