Goma yakabiliwa na uhaba wa chakula baada ya volkano
24 Mei 2021Hali hiyo ya ukosefu ya chakula ni baada ya barabara kutoka Butembo kuelekea katika mji huo ambayo imefunikwa na tope la volkano huku Gavana wa mkoa huo wa kivu ya kaskazini akitangaza pia kusitishwa kwa shughuli zote za shule katika maeneo hayo.
Magala na masoko ya vyakula katika maeneo kadhaa hapa mjini Goma yameanza kushuhudia upungufu mkubwa wa vyakula tangu jana Jumapili siku moja tu baada ya mlipuko wa volkeno nyiragongo uliosababisha maelfu ya wananchi kuyatoroka makazi yao.
Soma pia: Mripuko wa Volcano wazua taharuki mjini Goma
Hata hivyo hali hiyo inayowatia wasiwasi mkubwa wakaazi wa Goma na raia wanaoishi katika wilaya ya nyiragongo iliyoteketea kwa asilimia kubwa na moto huo imetokana na kufunikwa kwa barabara muhimu inayosafirisha bidhaa kutoka Butembo hadi Goma.
Shule zasimamishwa
Usiku mzima wa Jumapili kuamkia Jumatatu mvua kubwa na mitetemeko ya ardhi iliendelea kuutikisa mji wa Goma hali iliyowalazimu raia wengi kulala nje haswa wale wanaoishi katika nyumba za matofali.
Licha ya kupungua kwa rangi nyekundu iliyokuwa ikionekana tangu Jumamosi kwenye mlima Nyiragongo na Nyamulagira, kwa sasa ni wingu kubwa la moshi uliochanganyika na majivu ndiyo ulioifunika milima hiyo ya moto.
Soma pia: Watu waanza kurejea mjini Goma baada ya Volkano kutulia
Katika tangazo lililotolewa mapema Jumatatu, serikali ya kijeshi ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini imepiga marufuku shuguli zote za shule na kuwataka wazazi kuwalinda majumbani watoto wao katika kipindi hiki ambacho idadi kubwa ya watoto wametengana na familia zao na wengine kukanyagwa.
Volkano hiyo ya Nyiragongo iliyoko umbali wa kilometa 10 kaskazini mwa mji wa Goma iliripuka mara ya mwisho mnamo 2002 na kuwauwa watu 250 huku wengine zaidi ya laki moja kupoteza makazi yao.