1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guardiola: Haaland atavunja rekodi ya ufungaji

24 Oktoba 2022

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola sasa anasema ni jambo ambalo halihitaji mtu kufikiria, kujua kwamba mshambuliaji wake Erlind Braut Haaland atavunja rekodi ya ufungaji magoli kwa msimu mmoja.

https://p.dw.com/p/4Id06
UEFA Champions League Manchester City vs FC Copenhagen
Picha: Lee Smith/Action Images via Reuters

 Haaland kwa sasa ana mabao 17 kwenye mechi 11 tu za ligi msimu huu na rekodi ya ufungaji mabao mengi kwa msimu inashikiliwa na wakongwe Andrew Cole na Alan Shearer waliofunga mabao 34 kila mmoja.

"Nafikiri anafurahia timu inaposhinda ila bila shaka washambuliaji wote niliowaona katika taaluma yangu kama Samuel Eto'o, David Villa, Lionel Messi, Lewandowski, Thomas Müller na Sergio Aguero, walikuwa na hamu ya kufunga magoli kila mara. Ni kawaida, kwa hiyo ni lazima iwe hivyo, ni lazima," alisema Guardiola.

Champions League | Manchester City v Borussia Dortmund
Kocha wa Manchester City Pep GuardiolaPicha: Carl Recine/Reuters

Hayo yakiarifiwa kocha wa Newcastle United Eddie Howe sasa anawataka wachezaji wake wawe na mwendelezo wa ushindi wa mechi kila wanapoingia uwanjani. Hii ni baada ya klabu hiyo kuruka hadi katika nafasi ya nne katika jedwali la Ligi Kuu ya England kufuatia ushindi wao mkubwa wa 2-1 nyumbani kwa Tottenham Hotspur hapo Jumapili.

"Sijui, tutakachofanya ni kujituma kwa ajili ya kufanikiwa. Wachezaji wako katika sehemu nzuri sana, hali ya wachezaji wanapokuwa pamoja ni nzuri na ni vizuri kuona furaha na umoja wa wachezaji na tutaendelea kujituma katika kila mechi," alisema Howe.

Arsenal bado wanaiongoza ligi hiyo licha ya msururu wao wa ushindi kutiliwa kikomo hapo jana walipokwenda Southampton na kulazimishwa sare ya bao moja.