Guinea ya Ikweta kuandaa Kombe la Afrika
14 Novemba 2014Guinea ya Ikweta ambayo ina utajiri wa mafuta na mojawapo ya nchi ndogo kabisa barani Afrika ikiwa idadi ya watu laki sita pekee, iliandaa kwa pamoja dimba la 2012 na jirani yake Gabon lakini sasa itachukua jukumu la kuwa mwenyeji binafsi wa mashindano hayo kuanzia Januari 17 hadi Februari 8.
Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF limesema uamuzi huo umechukuliwa kufuatia mkutano wa jana mjini Malabo baina ya Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang na Rais wa CAF Issa Hayatou.
Guinea ya Ikweta ilikuwa imepigwa marufuku katika hatua ya mechi za mwanzo mwezi Agosti kwa kupatikana na hatia ya kumshirikisha mchezaji asiyestahili kucheza. Mechi za AFCON zitachezwa katika miji minne, Bata, Ebebiyn, Mongomo na mji mkuu Malabo. Droo ya mashindano hayo itafanyika mjini Malabo mnamo Desemba 3.
Morocco ilipigwa marufuku katika Kombe hilo baada ya kusisitiza kuwa mashindano hayo yanayotarajiwa kuandaliwa mwaka wa 2015 yaahirishwe, ikitoa sababu ya kitisho cha kusambaa ugonjwa hatari wa Ebola.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohamed Khelef