Guinea:Waandamanaji wa upinzani wasiopungua kumi wauliwa
23 Machi 2020Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Guinea baada ya kura ya amaoni na uchaguzi wa bunge ulighubikwa na ghasia zilizosababisha vifo vya watu wasiopungua 10 kulingana na upinzani nchini humo.Licha ya kuripotiwa na visa vya ugonjwa wa Corona,serikali ya Guinea iliitisha uchaguzi huo ambao unalenga kubadili katiba ilikuondowa uwingi wa mihula ya rais na kumuezesha rais wa sasa Alpha Conde kuwania muhula wa tatu.
Upinzani unaelezea kwamba watu wasiopungua 10 waliuliwa na maafisa wa usalama ,huku serikali ikielezea kwamba ni watu wanne waliouliwa kwenye machafuko yaliyotokea Jumapili wakati wa uchaguzi. Afisa mmoja wa upinzani amesema kwamba waliokufa ni wafuasi wa upinzani ambao waliandamana kupinga kufanyika kura ya maoni.
Kwenye mji mkuu wa Conakry, baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifungwa mapema kufuatia ghasia. Vuguvugu la vyama vya upinzani na asasi za kiraia la FNDC, linalopinga kuweko na muhula wa tatu wa rais Alpha Konde, linaelezea kwenye taarifa yake kwamba wanajeshi waliwafyetulia risasi waandamanji na kuwakamata baadhi ya wengine.
Vuguvugu hilo lilitisha maandamano mengine leo Jumatatu na kesho Jumanne ili kulazimisha kung'atuka madarakani rais Konde. Waandamanaji wasiopungua 32 wameuliwa tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita yalipoanza maandamano ya kupinga mageuzi ya katiba.
Rais Alpha Konde mwenye umri wa miaka 82 alichaguliwa mwaka 2010 na 2015, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo ambayo imeweka mihula miwili kwa uchaguzi wa rais.
Katiba inayopendekezwa hivi sasa pia inaweka mihula miwili lakini inampa mwanya rais wa sasa kugombea tena mara mbili. Uchaguzi wa rais umetarajiwa kuitishwa Oktoba, lakini uchaguzi wa hapo jana uliogomewa na upinzani utawapa nafasi wafuasi wa chama cha Conde kudhibiti wingi wa viti bungeni.
Idadi ya waliojitokeza kupiga kura haijafahamika,na mtandao wa intaneti ulikatwa. Nje kidogo ya mji wa Conaky vituo kadhaa vilichomwa moto na wandamanaji. Maafisa wameshuduia pia kwamba machafuko yalitokea pia katika mji wa Mamou, katikati mwa nchi, Boke magharibi mwa nchi na N´Zerekore kusini mashariki mwa Guinea.
Uchaguzi huo wa bunge na kura ya maoni uliakhirishwa kwa wiki tatu kufuatia machafuko yaliyosababishwa na maandamano ya upinzani.
Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa walisusia kushiriki kwenye mchakato huo wa uchaguzi kwa kile walichoelezea kwamba daftari la wapigaji kura halikuwa la kuaminika.
Marais wa nchi wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi, ECOWAS walifuta safari yao ya upatanishi dakika za mwisho kutokana mripuko wa ugonjwa wa Corona.