1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ahimiza ahadi zaidi kuokoa viumbe hai duniani

30 Oktoba 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezihimiza nchi kutoa ahadi mpya kusaidia kuokoa viumbe hai duniani na akatoa wito kwa sekta ya kibinafsi kuhusika katika juhudi hizo.

https://p.dw.com/p/4mNlb
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Amesema kila siku, dunia inapoteza spishi zaidi kutokana na uharibifu wa mazingiraPicha: Alexander Shcherbak/ITAR-TASS/IMAGO

Guterres amesema katika kauli zake za ufunguzi kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa bioanuai, unaofahamika kama COP16, mjini Cali, Colombia, kuwa mazingira ni uhai, na na bado yanapigwa vita, vita ambavyo havina mshindi.

Amesema kila siku, dunia inapoteza spishi zaidi. Mkutano huo wa kilele wa wiki mbili unafuatia muafaka wa kihistoria wa 2022 mjini Montreal, ambao unajumuisha hatua 23 za kuokoa maisha ya mimea na wanyama duniani.

Matamshi ya Guterres yamejiri siku moja baada ya mazungumzo kukwama kuhusu jinsi ya kufadhili uhifadhi wa mazingira. Serikali nane zimeahidi nyongeza ya dola milioni 163 kwa Mfuko wa Mfumo wa Bioanuai Duniani, ambao watetezi wa mazingira wanasema bado ziko mbali sana kuyafikia mabilioni yanayohitajika ili kuokoa viumbe hai duniani kote.