1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Guterres amtaka Biden kuiondolea vikwazo Iran

Daniel Gakuba
30 Juni 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemtolea wito Rais wa Marekani Joe Biden, kuondoa vikwazo dhidi ya Iran kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 2015 yaliyolenga kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/3voeM
Belgien Brüssel | Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: John Thys/AP/picture alliance

Rai hiyo ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa utawala wa Rais Joe Biden imetolewa wakati mazungumzo yakiwa yamefufuliwa baina ya wadau wa makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, yajulikanayo kwa kifupi kama JCPOA.

Soma zaidi: IAEA ina wasiwasi kuhusu vinu vya nyuklia vya Iran

Makubaliano hayo yanahusisha Iran kwa upande mmoja, na kwa upande nyingine zikiwemo nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama, yaani Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa pamoja na Ujerumani.

Mbali na kuitaka Marekani kuiondolea vikwazo Iran, Antonio Guterres pia ameitolea wito Iran kutekeleza kikamilifu majukumu yake yote chini ya makubaliano hayo.

Iran Atomprogramm
Iran imezidisha urutubishaji wa madini ya urani kama jibu kwa hatua ya Marekani kujiondoa makubaliano ya JCPOAPicha: Iranian Presidency Office/AP Photo/picture alliance

Ripoti mara mbili kila mwaka

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi 15 wanachama linatarajiwa kuijadili ripoti ya katibu mkuu wa Umoja huo ambayo huwasilishwa mara mbili kwa mwaka.

Makubaliano ya JCPOA yalisainiwa mwishoni mwa utawala wa Rais Barack Obama, Joe Biden akiwa makamu wake. Lakini Mrithi wa Obama, Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano hayo mwaka 2018, na kuimarisha tena vikwazo dhidi ya Iran.

Soma zaidi: Iran yailaumu Marekani kwa kuingilia masuala yake ya ndani

Iran ilijibu hatua hizo kwa kuongeza urutubishaji wa madini ya urani kutoka kiwango kilichokubaliwa cha asilimia 3,67 hadi asilimia 60, ikisogea karibu na urutubishaji wa asilimia 90 unaohitajika kutengeneza bomu la nyuklia.

Hata hivyo iran inaendelea kusisitiza kuwa malengo yake yanasalia kuwa ujenzi wa nishati ya atomiki kwa matumizi ya kiraia, na kuwa inaweza kurudi katika viwango vya awali vya urutubishaji ikiwa Marekani itaiondolea vikwazo.

USA PK President Donald Trump zum Atomabkommen mit Iran
Rais Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA mwaka 2019Picha: Reuters/J. Ernst

JCPOA njia pekee ya kuizuia Iran kupata bomu la nyuklia

Katika ripoti yake kwa baraza la usalama, Katibu Mkuu Guterres amesema anaendelea kuamini kwa dhati kuwa makubaliano ya JCPOA ndiyo njia muafaka ya kuhakikisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran utabakia katika mipaka ya nishati ya kiraia, ambayo matumizi yake ni ya amani.

Soma zaidi:Jeshi la Marekani lawashambulia wanamgambo Iraq na Syria

Huku hayo yakijiri, Marekani imeliarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi yake dhidi ya vituo vya wanamgambo washirika wa Iran ndani ya Irak na Syria, yalilenga kuwazuia wanamgambo hao pamoja na Iran kufanya mashambulizi zaidi dhidi maslahi ya Marekani na raia wake.

Chini ya kifungu nambari 51  cha mkataba wa Umoja wa Mataifa, taifa lolote linapaswa kuliarifu bila kukawia baraza la usalama kuhusu mashambulizi linaoyafanya katika juhudi za kujilinda.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema mashambulizi hayo ya mwishoni mwa juma lililopita yalifanywa baada ya juhudi nyingine zisizo za kijeshi kuambulia patupu.

 

rtre