1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterrres amwambia Haftar hakutakuwa na suluhisho la kijeshi

Yusra Buwayhid
2 Julai 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amemwambia kamanda wa vikosi vya mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, kuwa hakutakuwa na suluhisho la kijeshi katika mzozo wa Libya.

https://p.dw.com/p/3eg7C
Antonio Guterres bei einer Pressekonferenz in Äthiopien
Picha: AFP via Getty Images

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema Kamanda Haftar alimpigia simu Guterres Jumatano na walijadili maendeleo ya nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. Mwezi uliopita, wanajeshi wa Haftar walilazimika kurudi nyuma kutoka mji mkuu Tripoli ilipo serikali ya umoja wa kitaifa, GNA.

Kulingana na Dujarric, katibu mkuu huyo amemwambia Haftar kwamba suluhisho linaweza tu kuwa la kisiasa, ambalo litasimamiwa na Walibya wenyewe. Guterres pia amesisitiza pendekezo la Umoja wa Mataifa, la kutaka kufanyike mazungumzo kati ya pande hizo mbili kupitia Tume ya Pamoja ya Kijeshi ya Libya.

Aidha msemaji huyo ameeleza mshtuko wa Guterres baada ya kugunduliwa makaburi ya watu wengi katika maeneo yaliyopokonywa vikosi vya Haftar hivi karibuni. Guterres amesisitiza haja ya kuheshimiwa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu pamoja na sheria ya kimataifa ya ubinadamu.

Libyen Kämpfer der GNA
Wapiganaji tiifu kwa serikali ya Libya ya GNA, eneo la al-Sawani kusini mwa Libya, Tripoli.Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Guterres pia alizungumza na waziri mkuu wa Libya anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Fayez Serraj, ambaye aliashiria dhamira yake ya kufanya mazungumzo ya ndani ya Tume ya Pamoja ya Kijeshi nchini Libya na akaeleza nia yake ya kutafuta suluhisho la kisiasa kupitia uchaguzi.

Ufaransa na Uturuki zaendelea kuzozana juu ya Libya

Wakati huo huo, Ufaransa imesema Jumatano, kwamba itasimamisha kwa muda ushiriki wake katika operesheni ya kulinda usalama kwenye bahari ya Mediterania ya jeshi la jumuiya ya kujihami ya NATO kutokana na vitendo vya Uturuki, katika ongezeko jipya la mzozo uliozuka kati ya washirika hao wawili wa jumuiya hiyo ya kujihami.

Katikia siku za hivi karibuni, Ufaransa na Uturuki zimekuwa zikishambuliana juu ya mzozo wa Libya, huku kila upande ukimnyooshea mwenzake kidole cha lawama katika kuchochea umwagikaji damu kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Watu 30 wauawa Libya kwa mabomu ya ardhini

Wizara ya ulinzi imesema Ufaransa haitashiriki tena katika operesheni hiyo ya NATO hadi pale itakapopata jibu kutokana na wasiwasi wake kuhusiana na vitendo hivyo vya Uturuki.

Mwezi uliopita, Ufaransa ilidai kwamba meli za Uturuki ziliingilia kati meli za Ufaransa zilizokuwa zikishiriki katika ujumbe wa NATO kwenye bahari ya Mediterania, madai ambayo Uturuki inayataja kuwa hayana msingi.

Soma zaidi:Macron azikosoa Uturuki, Urusi mzozo wa Libya

Uturuki inaiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa katika mgogoro huo wa Libya, dhidi ya vikosi vya uasi vya Khalifa Haftar.

Ufaransa inatiliwa shaka na wachambuzi kuwa inamuunga mkono kamanda Haftar, ikishirikiana na Misri, Urusi na Umoja wa Falme za Kiarabu, lakini taifa hilo la Ulaya linasisitiza kuwa halielemei upande wowote katika mzozo huo.

Vyanzo: (ap,afp)