1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres asema kushambulia Rafah itakuwa janga la kibinadamu

7 Mei 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitolea wito Israel na Hamas kuongeza juhudi ili kufikiwe mkataba wa amani.

https://p.dw.com/p/4fb1H
Mkuu wa UN Antonio Guterres akizungumza katika Baraza la Usalama
Ameionya Israel kuwa kuishambulia Rafah "itakua kosa la kimkakati, janga la kubwa kwa binadamu."Picha: Yuki Iwamura/AP Photo/picture alliance

Hayo yanajiri wakati Hamas imetangaza kukubali pendekezo la usitishwaji mapigano lililotolewa na Misri na Qatar. Lakini Israel imesema pendekezo hilo halikidhi matakwa yake muhimu. Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA amesema:

Soma pia: Israel yatwaa udhibiti wa mpaka wa Rafah

"Asubuhi ya leo ilikuwa ni moja kati ya siku mbaya katika janga hili lililodumu kwa miezi saba. Jana, sote tulishuhudia picha za watu huko Gaza wakisherehekea, watoto wakicheza mitaani, wakiamini kwamba, baada ya muda mrefu, hatimaye kumefikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano. Hii ikimaanisha ni mwisho wa vita na hakuna tena ndugu au wazazi wao watakao kufa au kuhamishwa. Na huenda wangeweza kurudi nyumbani. Lakini ghafla matumaini yao yote yalitoweka baada ya kusikia kuwa hakuna usitishaji wa vita. Haifikiriki ni kiasi gani taarifa hii inaweza kukatisha tamaa."

Misri imewapokea wajumbe kutoka Qatar, Marekani, na wale kutoka kundi la Hamas ili hatimaye kutafuta njia ya kufikia mkataba wa amani huko Gaza. Israel imesema pia kuwa iko tayari kuwatuma wajumbe wake kwenye vikao hivyo vya upatanishi.