Guterres azirai Marekani na China kurekebisha mahusiano yao
20 Septemba 2021Guterres ametahadharisha kwamba mvutano baina ya madola hayo mawili yenye nguvu unatishia uwezekano wa kuzuka enzi mpya ya vita baridi.
Kwenye mahojiano maalumu na shirika la habari la Associated Press Guterres amesema kupwaya kwa mahusiano kati ya Washington na Beijing ni kitisho kwa usalama wa dunia hasa iwapo mivutano iliyopo baina ya madola hayo mawili itavuka mpaka na kuyahusisha mataifa mengine ulimwenguni.
Soma pia: China, Marekani zinapaswa kujitahidi kupunguza wasiwasi katika uhusiano wa kibiashara
Matamshi ya Guterres yanakuja katika wakati viongozi wa dunia wanakwenda mjini New York,Marekani kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa unaoanza kesho chini ya kiwingu cha janga la virusi vya corona, athari za mabadiliko ya tabianchi na mizozo kwenye maeneo mbalimbali duniani.
Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Marekani na China hazina budi isipokuwa kufanya kazi pamoja kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, biashara na teknolojia licha ya tofauti kubwa baina yao yanapokuja masuala ya haki za binadamu, uendeshaji uchumi, usalama na umiliki wa bahari ya China kusini.
China yaonya uhusiano mbaya na Marekani utarudisha nyuma mazungumzo ya hali ya hewa
"Kutokana na tofauti zote hizi, jambo moja liko wazi, tunayo sayari moja tu na mataifa yote haya yana nguvu kubwa kiasi yamefikia uhasama unaweza kuteteresha uwezo wetu wa kushughulikia changamoto za ulimwengu zinazozotukabili," amesema Guterres.
Pamoja na mambo mengine Guterres amekumbusha kuwa dunia haiwezi kukabiliana na changamoto lukuki zilizopo bila ya kuwepo mahusiano rafiki ndani ya Jumuiya ya Kimataifa na zaidi ya yote miongoni mwa madola yenye nguvu.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa Guterres kuonesha wasiwasi juu ya athari za kudorora kwa mahusiano kati ya Washington na Beijing na kitisho kilichopo cha kurejea enzi ya vita baridi iliyoihusisha wakati huo Marekani na uliokuwa muungano wa kisovieti ambazo kila moja iliongoza kundi la mataifa washirika kutunishiana misuli huku zikitumia silaha za nyuklia kama kinga dhidi ya mashambulizi.
Miaka miwili iliyopita mtendaji huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa aliwatahadharisha viongozi wa dunia juu ya hatari ya ulimwengu kugawika vipande viwili kwa Marekani na China kuunda mifumo kinzani ya sarafu, biashara, intaneti, kanuni za usimamizi wa fedha na hata mikakati ya kijeshi kwenye mataifa ambayo madola hayo mawili yana ushawishi mkubwa.
Katika mahojiano na shirika na Associated Press Guterres amerejelea wito wa kuhakikisha mahusiano ya Marekani na China yanasawazishwa na ulimwengu ni sharti uepuke vita nyingine baridi kwa gharama yoyote.
Ama kuhusu mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Guterres amesema viongozi watajadiliana masuala mengi ikiwemo hatua ziada za kuchukua kupambana na janga virusi vya corona, mabadiliko ya tabia nchi na hata hatma ya Afghanistan chini ya utawala mpya wa kundi la Taliban.