Guterres: jeshi la kimataifa linapaswa kupelekwa Haiti
25 Aprili 2023Katibu Mkuu Antonio Guterres alitoa wito wa dharura kwa ajili ya kupelekwa kikosi maalum cha wanajeshi nchini Haiti, kufuatia ombi mwezi Oktoba la Waziri Mkuu Ariel Henry na Baraza la Mawaziri la serikali ya Haiti. Lakini katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Januari hakuna nchi ilioonyesha utayari wa kupeleka wanajeshi wake nchini Haiti.
Guterres alisisitiza katika ripoti yake kwa Baraza la Usalama iliyosambazwa Jumatatu kwamba kupeleka kikosi cha kimataifa bado ni muhimu ili kusaidia mamlaka ya Haiti kuzuia vurugu na ukiukaji wa haki, kurejesha utawala wa sheria, na kuunda mazingira ya kuandaa uchaguzi wa kitaifa. Baraza la Usalama limepanga kujadili ripoti hiyo kesho Jumatano.
Jeshi la Polisi la Kitaifa nchini Haiti linakabiliwa na ongezeko la mashambulizi ya magenge ambayo yanachangia maafisa kadhaa wa polisi kususia au kutoroka majukumu yao. Antonio Guterres amesema tangu mwanzo mwa 2023, maafisa wa polisi 22 wameuawa na magenge, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kasi endapo jitihada hazitaongezwa maradufu kwa kuwapa polisi vifaa na kutoa mafunzo kwa haraka, na kuboresha mazingira ya kazi.
Hali mbaya ya kibinadamu
Msemaji wa Umoja wa Mataifa,Farhan Haq anasema hali ya kibinadamu huko Haiti imefikia viwango vya kutisha.
''Taarifa tulizonazo kutoka Haiti, ambapo hali ya usalama na kibinadamu katika maeneo mengi imefikia viwango vya kutisha. Kulingana na wenzetu wa mashirika ya kibinadamu, kati ya Aprili 14 na 19, mapigano kati ya magenge hasimu yalisababisha vifo vya karibu watu 70, wakiwemo wanawake 18 na watoto wasiopungua 2. Watu wengine 40 walijeruhiwa.", alisema Haq.
Jana Jumatatu, watu 13 wanaoshukiwa kuwa wahalifu wa genge waliuliwa kwa kuchomwa moto na umati wa watu katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Mgogoro wa kisiasa
Tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mnamo Julai 2021, magenge ya Haiti yamekua na nguvu na jeuri zaidi. Mnamo Desemba, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwa magenge yalidhibiti asilimia sitini ya mji mkuu wa Haiti, lakini wengi watu mitaani huko Port-au-Prince wanasema takwimu hizo zinakaribia asilimia mia moja.
Kwa upande wa kisiasa, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema hatua za kushughulikia vurugu za magenge nchini Haiti lazima ziambatane na hatua madhubuti za kutatua mgogoro wa kisiasa.