Gwajima ahojiwa na kamati ya bunge Tanzania
23 Agosti 2021Miongoni mwa tuhuma mbalimbali zinazomkabili mbunge huyo wa Jimbo la Kawe kupitia CCM Askofu Josephat Gwajima na hivyo kupelekea kuitwa na kamati hiyo ya bunge ni kudaiwa kusema uongo pamoja na kushusha hadhi na heshima ya bunge.
Awali Gwajima aliwasili majira ya saa 6 mchana akiwa katika gari nyeusi tofauti na gari anayotumia wakati akiwa bungeni na alipofika katika geti kubwa linalotumiwa na wabunge alipokelewa na askari wawili mmoja akiwa amevalia nguo za Polisi na mwingine nguo za kiraia.
Gwajima akiwa ameongoza na askari hao alielekezwa kukaa katika viti vilivyopo kwenye moja ya maeneo ya kumbi za mikutano bungeni hapo huku akisubiriwa kuitwa kuhojiwa na kamati ya Kudumu ya Bunge, haki, maadili na madaraka ya bunge.
Gwajima amekuwa akitoa kauli zinazokinzana na msimamo wa chama chake
Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo dhidi ya mbunge Josephat Gwajima, Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge haki, maadili na madaraka ya bunge Emmanuel Mwakasaka, amesema tayari kamati yake imemhoji kwa tuhuma zinazomkabili na kwamba shauri hilo litaendelea kusikilizwa kesho kutwa Jumatano.
Josephat Gwajima ambaye ni Askofu wa madhehebu ya kanisa la uzima na ufufuo duniani lakini pia ni mbunge kutoka chama tawala cha CCM, hata hivyo katika siku za hivi karibuni amekuwa akitoa kauli zinazokinzana na msimamo wa chama chake na serikali hususani katika suala zima la chanjo ya Covid 19.
soma zaidi:Viongozi wa dini Tanzania kupigia chapuo chanjo ya Covid-19
Gwajima amekuwa akisema kuwa yeye na waumini wa kanisa lake hawatachanjwa chanjo hiyo hadi hapo wizara ya afya itakapotoa elimu na ufafanuzi wa kina kuhusiana na madhara ya chanjo hiyo.
Hadi hivi sasa Tanzania imepokea dozi milioni moja ya Covid 19 aina ya Johnson and Johnson huku zoezi la utoaji chanjo hiyo likiendelea kwa mtu aliye tayari kuchanja.
Mwandishi:... Deo Kaji Makomba