1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Habari za kutatanisha kumhusu rais wa Gabon

Oumilkher Hamidou8 Juni 2009

Eti eti eti zimeenea kama rais wa Gabon yuhai

https://p.dw.com/p/I5Wk
Rais Omar Bongo (kati na miwani)Picha: AP


Libreville,mji mkuu wa Gabon,umejiinamia tangu jana usiku hakuna mtu njiani ,tangu vyombo vya habari vya Ufaransa kutangaza kwamba rais wa Gabon,Omar Bongo Ondimba amefariki dunia.Baada ya muda mrefu wa kutosema chochote,waziri mkuu wa Gabon Jean Eyeghe Ndong amezisuta habari hizo katika taarifa aloitoa hivi punde kutoka hospitali ya Quiron ya Barcelona .

Kumekua na habari za kutatanisha usiku kucha jana kuamkia leo hadi hivi punde,pale waziri mkuu Jean Eyeghe Ndong alipozisuta habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya Ufaransa.

"Tumejionea wenyewe kwamba rais wa jamhuri ya Gabon,Omar Bongo Ondimba yuhai",amesema waziri mkuu huyo na kuongeza yeye mwenyewe na mawaziri kadhaa wa serikali yake paamoja na spika wa bunge , wamemtembelea rais Omar Bongo leo asubuhi.

"Rais Omar Bongo hajafa",habari tulizozipata zinasema yu hai" duru kutoka wizara ya mambo ya nchi za nje ya Hispania zimesema.

Waziri mkuu wa Gabon amesema nchi yake itatuma malalamiko rasmi kwa serikali ya Ufaransa,dhidi ya ripoti za upotofu zinazotangazwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya Ufaransa.

Mtandao wa jarida la Ufaransa Le Point ulikua wa mwanzo kuzungumzia juu ya kifo cha rais Omar Bongo Ondimba.

Rais Bongo amelazwa hospitali mjini Barcelona nchini Hispania tangu mapema mwezi uliopita.Wakati ule viongozi wa Gabon walisema rais Bongo amekwenda kwa uchunguzi na kwamba "anasitisha kwa muda shughuli zake zote".Duru nyengine lakini zilisema rais Omar Bongo anaugua maradhi ya cancer ya matumbo.

Rais Omar Bongo Ondimba wa Gabon amekua akiitawala Gabon tangu miaka 41 iliyopita.

Mara baada ya televisheni na Radio za Ufaransa kutangaza habari hizo za kutatanisha,maduka, mikahawa na mabaa yalianza kufungwa na pirika pirika za kimaisha mjini Libreville kuanza kupwaya.

"Watu wanaogopa" amesema mfanyakazi mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe.

Madereva wa Taxi ambao wengi wao ni wageni,"wanakwepa kuingia katika eneo la kati la mji mkuu wakihofia kukaguliwa "-amesema hayo dereva mmoja aliyehojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Pekee vituo vya petroli ndivyo vilivyojazana umati wa watu wanaopiga foleni kujaza magari na kununua mafuta ya akiba kwaajili ya matumizi ya nyumbani.

Eti eti zimezagaa kuhusu nani atakabidhiwa hatamu za uongozi pindi habari za kufariki dunia Omar Bongo zikithibitishwa.

Mwanawe wa kiume,waziri wa ulinzi Ali Ben Bongo,anatajikana kua na nafasi nzuri ya kukabidhiwa hatamu za uongozi wa nchi hiyo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman