Habari za ulimwengu-dunia yetu leo jioni kutoka radio DW mjini Bonn
31 Januari 2005Waziri mkuu wa Iraq Iyad Allawi amewatolea mwito wairaq waungane na kuijenga upya nchi yao.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan ameilaumu vikali Sudan kwa kuziendeya kinyume haki za binadaam huko Darfour
Na marais wa Rashia na Palastina wamehimiza silaha ziwekwe chini na kufufuliwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina.
Baghdad:
Waziri mkuu wa Iraq Iyad Allawi ameutaja uchaguzi wa jana nchini humo kua ni ushindi dhidi ya magaidi.Akizungumza na waandishi habari waziri mkuu Iyad Allawi amewashukuru wanajeshi wa nchi shirika na wananchi kwa kufanikisha uchaguzi huo.Waziri mkuu wa serikali ya mpito ametoa mwito wa umoja wa taifa,akisema wairaq wote,mamoja wamepiga kura au la,wanabidi washirikiane kuijenga Iraq mpya.Naibu mwenyekiti wa kamisheni ya uchaguzi Hareth Mohammed Hassan amesema asili mia 60 hadi 75 ya wairaq wametoa sauti zao.Na huku matokeo ya uchaguzi yakisubiriwa,vyama 2 vya wakurd vilivyounda muungano katika maeneo ya kaskazini ya Iraq vimesema vinaongoza katika eneo hilo linalojitawala wenyewe.Matokeo ya hadi sasa yanaonyesha chama cha kidemokrasi cha Kurdistan na Umoja wa wazalendo wa Kurdistan vinaongoza HUKO Suleimaniya na Erbil.Licha ya sifa na pongezi za walaimwengu kwa uchaguzi wa Iraq,baraza la maulamaa wa Iraq-linabisha uhalalifu wa uchaguzi huo.Msemaji wa baraza hilo la waumini wa madhehebu ya sunni,Sheikh Omar Ragheb anasema idadi ya waliopiga kura ni ndogo kuliko ile inayotajwa.Matokeo rasmi ya uchaguzi wa Iraq yanatazamiwa kutangazwa kati kati ya wiki ijayo.
Washington:
Rais George W. Bush wa Marekani ameutaja uchaguzi wa kwanza huru kuitishwa Iraq baada ya miaka 50,kua ni ufanisi.Amesema wairaq wamedhihirisha wanataka demokrasia.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan amesema wakati wa suluhu umewadia.Amewatolea mwito wairaq wa jamii ziote waashirikiane kubuni katiba mpya.Waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair ameutaja uchaguzi huo kua ni pigo kwa magaidi.Mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya,Jean Asselborn ameshadidia wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje mjini Brussels,wairaq wameonyesha ujaasiri,walipopuuza onyo la magaidi na kuteremka vituoni kupiga kura.Serikali ya shirikisho mjini Berlin imeutaja uchaguzi huo wa iraq kua ni hatua muhimu kuelekea demokrasia.Katika nchi za Ghuba maoni ya wahariri yanatofautiana.Kuna wanaosifu uchaguzi huo na wengine wanaouangalia kwa jicho la tahadhari.
Baghdad/London:
Vikosi vya usalama vya Iraq vimewakamata watuhumiwa wasiopungua 200 kuhusiana na mashambulio ya jana ambapo watu wasiopungua 39 wameuwawa .Watuhumiwa wanne ni wageni wenye uraia wa kiarabu-amesema waziri wa mambo ya ndani Falah al Bakib.Waziri huyo wa mambo ya ndani ameongeza kusema waasi wanne wameuliwa na vikosi vya usalama jana.Wakatui huo huo kundi la itikadi kali la Ansar al Islam limesema linahusika na kuanguka ndege ya kijeshi ya Uengereza Hercules nambari C-130 iliyokua ikielekea Balad kaskazini mwa Baghdad.Wizara ya ulinzi ya Uengereza imesema hii leo wanajeshi 10 wameuwawa ndege hiyo ilipoanguka.
Abuja:
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan ametoa mwito wa kuimarishwa mafungamano kati ya Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika,kuweza kuyafikia malengo ya Millenium hadi ifikapo mwaka 2015.Akihutubia mbele ya viongozi wa umoja wa Afrika mjini Abuja,katibu mkuu Kofi Annan amesema bara la Afrika liko mbali na kuyafikia malengo hayo-lakini yanawezekana,amesisitiza katibu mkuu wa umoja wa mataifa ikiwa jumuia ya kimataifa itawajibika kamataifa itawajibika kama ilivyoahidi.Ameshadidia ufunguo wa ufanisi ni pale umoja wa mataifa utakaposhirikiana kwa dhati zaidi na umoja wa Afrika.Pembezoni mwa mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa afrika,katibnu mkuu Kofi Annan alizungumzia haja kwa umoja wa mataifa kuzingatia uwezekano wa kuiwekea vikwazo Sudan.Katibu mkuu Kofi Annan ameilaumu Sudan kwa kuziendeya kinyume haki za binadam katika jimbo la magharibi la Darfour.Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekua wakikutana Abuja kwa kikao chao cha nne ambapo miongoni mwa mengineyo walizungumzia juu ya mizozo ya bara la Afrika na umuhimu wa kutumwa wanajeshi wa kulinda amani katika maeneo ya mizozo.Mkutano wa akilele wa Umoja wa Afrika ulianza kwa viongozi kukaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa gharika ya Tsunami iliyopiga Asia na mashariki ya Afrika.
Kuweit:
Watu wasiopungua watano wameuwawa katika opereshini nyengine dhidi ya magaidi mjini Kuweit.Shirika la habari la Kuna limesema vikosi vya usalama vimelivamia jumba moja kusini mwa mji mkuu huo ambamo wanamgambo wa kiislam wanasemekana wamejificha.Watu watatu waliuwawa jana katika opereshini kama hiyo mjini Kuweit.Hii ni mara ya nne kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa vikosi vya usalama kuwaandamana wanamgambo wa itikadi kali mjini Kuweit-taarifa ya wizara ya ndani imesema.Wanamgambo hao wanatajikana kua na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida.Duru za kuaminika zinasema vikosi vya usalama vinawasaka dazeni moja zaidi ya wanamgambo wa kiislam waliojificha katika mtaa wa Mubarak al Kabir kusini mwa Kuwerit City.
Ntulele-Kenya:
Mapigano mepya kati ya wafugaji wa kimasai na wakulima wa ki-kikuyu yamegharimu maisha ya mtu mmoja na webgine kujeruhiwa.Watu mamia kadhaa wameyahama maskani yao.Habari hizo zimetangazwa na madhamana wa Kenya hii leo.Mapigano hayo yameripotiwa kutokea mwishoni mwa wiki iliyopita umbali wa kilomita mia moja kusini magharibi ya mji mkuu Nairobi.Mkuu wa polisi katika eneo hilo la machafuko John Egesa amekiri mbele ya ripota wa shirika la habari la reuters,machafuko kati ya wamasai na wakikuyu yanaathiri shughuli za uchumi za eneo hilo.
Moscow:
Rashia inaunga mkono hatua zilizochukuliwa na rais wa Palastina Mahmoud Abbas kukomesha mapambano kwa mtutu wa bunduki katika mashariki ya kati."hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja kati ya Rashia na Palastina iliyotiwa saini na marais Vladimir Putin na Mahmoud Abbas hii leo huko Kremlin.Viongozi hao wawili wameelezea umuhimu wa kuanzishwa haraka mazungumzo kati ya Israel na Palastina na kufungua njia ya kushirikiana katika sekta ya usalama .Taarifa hiyo imeelezea pia umuhimu wa kutiwa njiani mpango wa pili wa amani ulioandaliwa na Marekani,rashia,Umoja wa mataifa na umoja wa ulaya.Wakati huo huo viongozi wa utawala wa ndani wa Palastina wamesema msichana wa miaka 10 ameuliwa hii leo na jeshi la Israel akiwa katika shule ya kambi ya wakimbizi ya Rafaa huko Gaza..