Dikteka Habre apatikana na hatia
30 Mei 2016Dikteta huyo wa zamani alipewa adhabu hiyo kwenye mahakama maalumu ya mabaraza ya Afrika, katika mji mkuu wa Senegal, Dakar. Jaji Gberdao Gustave Kam alisema wakati wa kuitoa hukumu hiyo.
"Kutokana na hayo Hissene Habre, mahakama inakuhukumu kifungo cha maisha jela."
Nderemo baada ya hukumu kutolewa
Mamia ya watu walishangilia baada ya Habre kupewa adhabu hiyo mjini Dakar. Waliokuwa wafungwa wakati wa utawala wake walikumbatiana kwa furaha kubwa huku wenye magari wakipiga honi!
Habre alipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya maalfu ya watu wakati wa utawala wake kuanzia mwaka wa 1982 hadi 1990.
Tume ya ukweli iliyoundwa mnamo mwaka wa 1992 nchini Chad imemlaumu dikteta huyo wa zamani kwa kuweka mfumo wa mateso na imesema kwamba watu 40,000 waliuawa wakati wa utawala wake. Tume hiyo imelinyooshea kidole hasa jeshi la polisi.
Habre ameishutumu hukumu iliyotolewa dhidi yake na amesema imetokana na sababu za kisiasa. Habre na wafuasi wake, mara kadhaa walijaribu kufanya fujo mahakamani kwa kupiga kelele na kuimba.Hapo awali alikataa kutetewa na mawakili lakini mahakama iliwateua wanasheria wa Senegal ili wamtetee.Habre amekuwa anaishi nchini humo tangu akimbie Chad mnamo mwaka wa 1990.
Deby aunga mkono hukumu
Rais wa Chad Idris Deby aliekuwa mshauri wa masuala ya kijeshi wa dikteta Habre,kabla ya kumtimua madarakani ,ameunga mkono adhabu iliyotolewa na mahakama.
Kesi ya Habre imefanyika kutokana na juhudi za watu waliofungwa jela wakati wa utawala wake. Watu hao wamekuwa wanaendesha kampeni ya kumfikisha mahakamani.
Wakili wa asasi ya haki za binadamu ya Human Rights Watch, Reed Brody ameeleza kwamba Habre alifikishwa mahakamani siyo kutokana na juhudi za waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa,ICC ya mjini the Hague na wala siyo kutokana juhudi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bali ni kutokana na juhudi za watu wa Chad wenyewe waliokumbwa na uhalifu uliotendwa na dikteta huyo wa zamani.
Kesi hiyo iliyosikilizwa na mabaraza maalumu ya Afrika na kufanyika nchini Senegal ilianza mnamo mwezi Julai mwaka uliopita.
Hii ni mara ya kwanza kwa mtawala wa zamani kuhukumiwa na mahakama za nchi nyingine kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mahakama maalumu iliyosikiliza kesi ya Habre iliundwa na Senegal kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika. Kesi nyingine juu ya fidia kwa kwa asasi za kiraia zaidi ya 4000 itafanyika katika siku zijazo.
Mawakili wa Habre wanazo siku 15 za kukata rufani.
Mwandishi: Mtullya Abdu/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef