1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti lazima ifanye maamuzi sasa

11 Januari 2011

Magazeti ya leo (11 Januari 2011) yanazungumzia mgongano katika Chama cha Christian Social Union (CSU), duru ya pili ya uchaguzi nchini Haiti na kile kinachoonekana kama kuibuka kwa siasa mpya za chuki nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/zwCJ
Haiti baada ya tetemeko la ardhi mwaka jana
Haiti baada ya tetemeko la ardhi mwaka janaPicha: AP

Gazeti la Leipziger Volkszeitung linazungumzia mgongano wa maneno kati ya wanasiasa wawili wa ngazi ya juu katika chama cha CSU, Waziri wa Ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg, na Franz Josef Strauß. Strauß aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, mwanasiasa hawezi kuwa maarufu kuliko chama, vyenginevyo awe ni kupe. Na maneno haya hasa, yanatajwa kwamba alimkusudia zu Guttenberg. Sasa naye zu Guttenberg ananukuliwa na gazeti hili, akijibu: "Lau ningelikuwa nimeamua kuishi maisha ya kupe, basi ningelikuwa chawa au mbu." Naye pia akimkusudia Strauß. Wakubwa wana mambo, anasema mhariri wa Leipziger Volkszeitung.

Mwezi mmoja baada ya uchaguzi, bado hakujawa na Rais
Mwezi mmoja baada ya uchaguzi, bado hakujawa na RaisPicha: AP

Gazeti la Neue Osnabrücker linazungumzia hali ilivyo nchini Haiti, nchi ambayo imekuwa ikikumbwa na majanga juu ya majanga. Kwanza ulikuwa ufukara, likaja tetemeko la ardhi na hivi karibuni wakawa na kipindupindu na sasa ni machafuko yanayotokana na uchaguzi, na, bila ya shaka, hali ya kuvunjika moyo miongoni mwa wananchi wa huko.

Mhariri anaisikitikia nchi hii, ambayo anasema inazidi kuzama kwenye hali duni. Ni shida kupata habari njema kutoka nchi hii. Ni kama kwamba, imeandikiwa ikwame hapo hapo ilipo isiende mbele, maana baada ya lile janga kubwa la tetemeko, makundi kibao yalijitokeza kuisaidia. Mamilioni ya pesa yakaahidiwa na misaada ikakusanywa. Lakini hadi leo, hakuna lolote la maana lililofanyika, zaidi ya hali ya maisha kuzidi kuwa mbaya.

Mhariri anasema kwamba umeshafika wakati sasa kwa Wahaiti kuamua kuwa na uongozi madhubuti unaoweza kuwazamua kwenye lindi hili la ufukara na hali ya kuvunjika moyo. Kwamba jamii ya kimataifa inaweza kusaidia pale tu wenyewe wanapoonesha njia.

Gabrielle Giffords
Gabrielle GiffordsPicha: dapd

Nayo tahriri ya gazeti la Lausitzer Rundschau inaendeleza hoja inayowahusisha wanasiasa wa kihafidhina nchini Marekani na kuibuka kwa wimbi la mashambulizi ya silaha dhidi ya wanasiasa wa mrengo wa kati, kama lile la mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya mbunge Gabrielle Giffords, huko Arizona.

Mhariri anasema kwamba, Sarah Palin anatamani kuikosha mikono yake. Binafsi inaweza ikawa ni kweli, si yeye aliyemchochea yule kijana wa miaka 22, kwenda kumjeruhi vibaya kwa risasi Giffords, na kuwauwa wengine sita, lakini kauli ambazo yeye, Palin, na wahafidhina wenzake wamekuwa wakizitoa kwa miezi mingi sasa, zilikuwa haziashirii kheri.

Kwa mfano kaulimbiu yake, inayoonekana pia kwenye mtandao wake, ikisomeka: "Usiweke chini bunduki yako, bali ijaze risasi" inaweza kuwa kichocheo cha tukio kama hili. Palin na wasiasa wenzake wa mrego wa kulia wa vuguvugu la Tea Party, wamekuwa hawakisii la kusema wanapoongea na wafuasi wao, na hivyo si ajabu kuwa matukio kama haya yanatokea sasa. Mhariri anamalizia kwa kuuliza: Hivi wenzetu Wamarekani munaelekea wapi?

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Mohammed Abdirahman