1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti yajitayarisha na kimbunga Issac

MjahidA25 Agosti 2012

Kituo cha kitaifa cha Marekani kinachoshughulikia maswala ya kimbunga kimesema kimbunga cha Issac kinatarajiwa kuikumba nchi ya Haiti.

https://p.dw.com/p/15wYO
Raia wa haiti wanaoishi katika mahema kuathirika na kimbunga Issac
Raia wa haiti wanaoishi katika mahema kuathirika na kimbunga IssacPicha: picture alliance / abaca

Jana jioni tayari mvua kubwa ilianza kunyesha katika Jamhuri ya Dominica iliyo katika kisiwa cha Hispaniola pamoja na Haiti.

Mafuriko na maporomoko ya udongo ambayo hutokea nchini humo kila wakati yanatarajiwa kuzidi kuwaathiri watu zaidi ya 400,000 ambao bado wanaishi katika mahema, baada ya tetemeko kubwa la ardhi la mwaka wa 2010 ambapo zaidi ya watu 250,000 waliuwawa.

Kituo hicho cha NHC kimesema Kimbunga Isaac kinatarajiwa kulikumba eneo la kusini mashariki mwa mji mkuu wa haiti Port-au-Prince na kitakuwa na upepo mkali utakaovuma kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa. Hata hivyo kimbunga hicho pia kinatarajiwa kuvuka na kuingia kusini Mashariki mwa Cuba usiku wa leo.

Wakati huo huo kumekuwa na milolongo mirefu nje ya maduka ya vyakula huku watu wakinunua vyakula hivyo ili kuvihifadhi nyumbani kufuatia kimbunga hicho. Rais Michel Martelly, aliyekatiza safari yake nchini Japan alitoa ushauri kwa raia wake kufuata ushauri wa wizara ya ulinzi.

Kwa upande wake waziri mkuu wa Haiti Laurent Lamothe, amesema serikali nzima ikiwemo vikosi vya usalama, imehamasishwa kujitayarisha kwa kimbunga hicho, waziri mkuu huyo amesema watafanya kazi pamoja na washirika wao ili kuona wanalidhibiti swala hili vilivyo.

Huku hayo yakiarifiwa Jeshi la Marekani imesema kesi ya watuhumiwa watano wa shambulio la Septemba 11 imeahirishwa hadi October kufuatia kimbunga Isaac katika eneo hilo.

Kesi hiyo ambayo mtuhumiwa Khalid Sheikh Mohammed alikiri kuhusika, sasa itasikilizwa October 15-19 katika kambi ya jeshi ya Marekani ya Guantanamo Bay nchini Cuba. Kesi hiyo awali ilikuwa imeairishwa kutoa fursa kwa washtakiwa kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, na sasa imesongezwa tena mbele kufuatia kimbunga Isaac ambacho kinahofiwa kukumba kusini mashariki mwa Cuba.

Mohammed anashtakiwa pamoja na mpwa wake raia wa Pakistan Ali Abd al-Aziz Ali, ambaye pia anajulikana kama Ammar al-Baluchi, wengine ni Mustapha al-Hawsawi raia wa Saudi Arabia na raia wa Yemen Ramzi Binalshib na Walid bin Attash.

Wote hawa huenda wakahukumiwa kifungo cha maisha iwapo watapatikana na hatia ya kuhusika na shambulio la mwaka wa 2001 ambapo kundi la kigaidi la Al Qaeda liliteka nyara ndege moja na kushambulia majengo mawili mjini New York Marekani. Watu 2,976 waliuwawa.

Mwandishi: Amina Aubakar/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo