Hakuna makubaliano kati ya Eu na Uingereza kuhusu Brexit
16 Septemba 2019Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker wameshindwa kufikia makubaliano yoyote kuhusu mpango wa Uingereza kujitowa katika Umoja wa Ulaya.Mkutano uliofanyika Luxembourg ni wa kwanza uliowakutanisha viongozi hao ana kwa ana.
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker na waziri mkuu Boris Johnson walikaa kwa muda wa masaa mawili wakijadiliana,mazungumzo ambayo yalionekana kuwa marefu katika wakati kukiwemo madai kutoka upande wa Uingereza kwamba makubaliano yanakaribia kufikiwa.
Tamko lililotolewa na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya baada ya kikao hicho ni kwamba Uingereza bado haijatowa mapendekezo yanayoweza kutekelezwa kisheria ambayo yanaweza kuwa suluhisho katika suala linalohusu mpaka wa Ireland ambalo ndio mzizi mkubwa wa fitna unaoweka kizingiti katika makubaliano ya Brexit.
Juncker amesisitiza ,kuhusu kuendelea kuwepo nia ya halmashauri ya Umoja wa Ulaya na uwazi katika kutathmini ikiwa mapendekezo yanafikia malengo ya kipengee kinachohusu mpaka wa Ireland, ambacho kimekataliwa na Uingereza. Taarifa ya Halmashauri ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa inasema mapendekezo hayo bado hayajawasilishwa na Uingereza lakini pia Umoja huo umesisitiza kwamba maafisa wake wataendelea kupatikana masaa 24 kwa siku kushughulikia suala hilo.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anasema Uingereza itajiondowa Umoja wa Ulaya kama ilivyopangwa Octoba 31 iwe ni kwa makubaliano au bila ya makubaliano. Lakini pia anasisitiza kwamba anaweza kufanikisha suala la kujadiliwa upya kwa makubaliano ya awali na Umoja wa Ulaya kwa wakati. Aidha, imeripotiwa kwamba Junker na Johnson wamekubaliana mazungumzo yanapaswa kushika kasi kutafuta mwafaka.
Katika makala ya gazeti la Telegraph toleo la Jumatatu waziri mkuu Johnson amenukuliwa akijionesha anaamini kwa dhati kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa na kuidhinishwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika Octoba-18.
Wakati Umoja wa Ulaya ukisema haujapokea mapendekezo ya Uingereza,msemaji wa waziri mkuu Boris Johnson ,James Slack anasema Uingereza imeshawasilisha mapendekezo ya kushughulikia maeneo kadhaa.
Ingawa pia hakutaka kutowa maelezo zaidi juu ya hilo akisema hakuna sababu ya kulijadili suala hilo hadharani.
Hata hivyo toka hapo hakuna upande wowote unaotarajia kufikia makubaliano ingawa mambo mengi bado yanategemea viongozi hawa Johnson na Juncker ambaye kwa hakika kama walivyo maafisa wengine wa Umoja wa Ulaya ameshachoshwa na mchezo wa kufukuzana unaochezwa na Uingereza na msimamo mkali unaoneshwa na Johnson. Mkutano wa leo ndio umeshafungua mwanzo wa wiki ya msuguano kuhusu suala hilo wakati zikiwa zimebakia siku 45 tu kufikia tarehe ya mwisho iliyowekwa Uingereza kupokea rasmi talaka yake.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Daniel Gakuba