1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haley: Kiongozi wa Palestina hana ujasiri wa mpango wa amani

Sylvia Mwehozi
26 Januari 2018

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kiongozi wa Palestina Mahmud Abbas anakosa ujasiri unaohitajika katika mpango wa amani.

https://p.dw.com/p/2rY4H
USA UN-Sicherheitsrat in New York - US-Botschafterin Nikki Haley
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Matthews

Haley aliyasema hayo muda mfupi baada ya rais Donald Trump kusisitiza kuwa Wapalestina "wameikosea heshima" Marekani na kutoa kitisho kipya cha kukata misaada wakati alipokutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Davos, Uswisi.

Marekani bado iko imara sana kwa mpango wa amani wa Palestina na Israel, alisema Haley, akiongeza kwamba hawako tayari kukimbizana na utawala wa Palestina ambao unakosa kile kinachohitajika kwa ajili ya upatikanaji wa amani. Zaidi Haley anasema.

"Licha ya yote haya, Marekani imejiandaa kikamilifu na ina  dhamira kutafuta amani. Hatujafanya chochote kuhusu mipaka ya mwisho ya Jerusalem. Hatujafanya chochote kubadilisha hadhi ya maeneo matakatifu. Tunabaki na nia ya  uwezekano wa mataifa mawili, ikiwa itakubaliwa na pande zote," alisema Haley.

Frankreich Abbas bei Macron
Kiongozi wa Palestina Mahmud AbbasPicha: Getty Images/AFP/F. Mori

Balozi huyo ambaye ameitetea kwa nguvu Israel katika Umoja wa Mataifa , amesema Abbas "amemtukana" Trump na kutaka kusitisha kutambuliwa kwa Israel baada ya uamuzi wa Marekani wa kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Alikuwa akimaanisha hotuba ya Abbas aliyoitoa Januari 14 kwa uongozi wa Wapalestina ambapo Abbas anaripotiwa kuwa alimdhihaki Trump na kumfokea juu ya fedha zake wakati akijibu vitisho vya Marekani vya kuikatia ufadhili Palestina.

Abbas pia alisitisha mkutano uliokuwa tayari umepangwa na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ili kupinga uamuzi wa Marekani juu ya Jerusalem, mji ambao Wapalestina wanauchukulia pia kama mji mkuu wa taifa lao la baadae.

Akilihutubia baraza la usalama, balozi wa Palestina Riyad Mansour amesema utafutaji wa amani umekuwa ni "kazi ya maisha" ya Abbas na kupendekeza kuwa mashambulizi dhidi ya kiongozi huyo wa Palestina ni aina ya "uovu".

USA Riad Mansur UN Sicherheitsrat in New York
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad MansourPicha: picture alliance/AP Photo

"Ni msimamo unaoheshimu haki za binadamu na utu wa watu wetu, ambao hatuwezi kuruhusu kufanyiwa ukatili. Hakuna gharama inayoweza kununua haki na utu wa raia. Hawawezi kutetereka na vitisho, na vitendo vya adhabu na mambo kama haya yanapaswa kukataliwa na wote wanaotafuta amani na haki, " amenukuliwa Mansour akisema.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kujadili mvutano baina ya Israel na Palestina kwa mara ya kwanza tangu Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ulivyopiga kura 128 kwa 9, pamoja na nchi 35 kutokuwepo kupinga uamuzi wa Marekani wa kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Hatua ya Marekani ilivunja makubaliano ya miongo kadhaa ya kimataifa kwamba hadhi ya mji huo inapaswa kutatuliwa kama sehemu ya mpango wa amani wa mataifa mawili baina ya Israel na Palestina.

Mkutano huo pia ulifanyika baada ya uamuzi wa Marekani wa kusitisha ufadhili wa zaidi ya dola milioni 100 kwa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Palestina UNRWA, hatua iliyokosolewa na serikali za Ulaya.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Saumu Yusuf