Hali Burkina Faso inatia wasiwasi
2 Desemba 2021DW imeripoti kuwa kundi la magaidi wenye mafungamano na al-Qaida la JNIM ambalo lilianzia nchini Mali, limeudhibiti mji huo kwa mara ya kwanza na kusababisha watu kukimbia huku makanisa yakifungwa.
"Wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi wanadhibiti kijiji," mkaazi mmoja ambae alikimbilia mji mkuu, Ouagadougou na anaeendelea kuwasiliana na jamaa waliobaki huko ameimbia DW na kuongeza kuwa "Ni wanawake, watoto na wazee pekee ndio wamesalia huko." Ingawa hakujapatikana uthibitisho rasmi, chanzo cha kuaminika katika taasisi za usalama kilithibitisha taarifa hiyo.
Matukio hayo yanaonyesha ni jinsi gani magaidi hao wanavyojizatiti kiurahisi katika eneo hilo. Kundi la JNIM limefanya mashambulizi maeneno ya kaskazini-magharibi, wakati kundi linalojiita Dola ya Kiislam katika ukanda mkubwa wa Sahara (ISGS) likiendesha harakati zake hasa mashariki na eneo la mpaka la nchi jirani ya Niger.
Wito wa rais Kabore kujiuzulu
Nchi yetu iko vitani, na inazidi kutoweka. Tayari tumekwisha poteza sehemu kubwa ya ardhi,” amesema Ibrahima Maiga, ambae sasa anaishi nchini Marekani na ndie mwanzilishi-mwenza wa vuguvugu la "Tuiokoe Burkina Faso".
Wito umekua ukitolewa kumtaka Rais Kabore kujiuzulu. Kwa wiki kadhaa, jumuiya ya kiraia imekuwa ikitoa shinikizo kubwa kwa serikali ya Kabore, ambayo imekuwa madarakani tangu 2015. Mwishoni mwa jumaa hili, vuguvugu la "Tuiokoe Burkina Faso" linapanga kuandaa maandamano mapya alisema Maiga.
"Tumeamua kuendelea kuandamana hadi kuwe na mabadiliko ya kweli. Na tunaona kuwa hakuna mabadiliko yoyote yanayoweza kupatikana kama Rais Kabore hatang'atuka madarakani. Ndiyo maana tunadumisha kasi hii ya maandamano," alisema Maiga.
Zaidi ya watu 2,000 wamekufa kutokana na ugaidi tangu 2016. Takriban watu 285 walifariki kati ya Julai na Septemba pekee, kwa mujibu wa shirika la kuhudumia watoto UNICEF. Watu wengine takriban milioni 1.5 wameyahama makaazi yao, takriban shule 2,700 zimefungwa, na zaidi ya watoto na vijana 300,000 hawapati tena elimu. Tishio la ugaidi ni mzozo mkubwa zaidi wa usalama tangu Burkina Faso ipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka wa 1960.
Shambulio ambalo lilibadilisha kila kitu na kichochezi cha shinikizo kubwa kwa serikali ni shambulio la Novemba 14 dhidi ya vikosi vya usalama huko Inata eneo la kaskazini karibu na mpaka wa Mali. Makundi ya kigaidi waliwauwa takriban wanajeshi 53 na raia wanne. Ni moja ya mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya vikosi vya usalama katika ukanda wa Sahel. Kwa raia wengi wa Burkina Faso kama Prosper Nikiema, hatimae magaidi walikuwa wamevuka mstari mwekundu. Alisema shambulio la kuvizia kwenye kituo cha polisi lilidhihirisha kuwa hali ni mbaya kwa muda mrefu sana.
Madai ya kuwepo serikali ya Umoja wa Kitaifa
"Bila shaka, kila mara kumekuwa na dalili za hatari. Lakini hizi hazijachukuliwa kwa uzito hata kidogo," Nikiema aliiambia DW. Kwake, pia, jambo moja tu ni la muhimu: kujiuzulu kwa Rais Kabore ambae anadhani hana ujasiri. Nikiema alipendekeza kuwa kuna haja ya kupata viongozi majasiri ambao wanaweza kupambana na ugaidi kwa ufanisi. Kwa mfano, kunahitajika operesheni ya kikanda ya kupambana na ugaidi.
Siku ya Jumanne, waziri wa usalama Maxime Koné alitangaza kuwa Ghana, Togo, na Ivory Coast zilishiriki katika operesheni kama hiyo yenye zaidi ya wanajeshi 5,700. Na walifanikiwa kuwakamata washukiwa wasiopungua 300 na kuwapokonya silaha haramu. Hata hivyo, operesheni hiyo ilipangwa kabla ya maandamano ya hivi majuzi.
Amadou Diemdioda Dicko, mbunge wa chama cha upinzani cha Umoja wa Maendeleo na Mabadiliko (UPC), anaamini kuwa mipango wa kikanda wa kupambana na ugaidi ni muhimu. "Hali hiyo ipo pia Mali na Niger," Dicko ameiambia DW na kuongeza kuwa "Watu wanapaswa kuelewa kwamba tunaweza tu kupambana na ugaidi kwa pamoja." Kwa maoni yake, sio jukumu la serikali tu: "Wananchi ni lazima wahusishwe pia, kwa mfano, wanaweza kuripoti watu wanaowatilia mashaka. Silaha pekee haziwezi kuleta suluhisho." alimalizia Mbunge Amadou Dicko.
Baadhi ya wadau wengine wa siasa nchini Burkina Faso wanadai kuwepo serikali ya umoja wa kitaifa licha ya kusema kuwa itakuwa vigumu kupata watu wa kuiongoza kutokana na kwamba serikali na upinzani ni kitu kimoja.
Eric Ismael Kinda, msemaji wa vuguvugu la wananchi la Balai Citoyen (Ufagio wa Mwananchi), anasema kuwabadili viongozi katika nyadhifa zao haitoshi. Badala yake, alisema, umahiri na utendaji mzuri vinahitajika.
Vuguvugu la Balai Citoyen ndilo liliongoza maandamano ya amani ambayo yalimlazimu Rais wa zamani Blaise Compaoré kujiuzulu mwaka 2014. Balai Citoyen imekuwa ikijivunia nguvu na msaada mkubwa kutoka kwa raia wa Burkina Faso.