Mashambulio yanapamba moto
15 Oktoba 2015Akiwahutubia wapalastina kwa mara ya kwanza tangu wimbi hili la machafuko lilipozuka wiki mbili zilizopita,kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahamoud Abbas amesema anaunga mkono "vuguvugu la amani" na kushadidia "haki yao ya kujihami" dhidi ya uvamizi wa Israel.
Mashambulio mengine mawili ya visu yameripotiwa jana jioni mjini Jerusalem;la kwanza dhidi ya afisa wa kikosi cha usalama,ambalo halikufanikiwa na la pili,likatokea karibu na kituo cha usafiri ambapo bibi mmoja alijeruhiwa-shambulio hilo lilizusha vurumai kubwa katika eneo hilo.Vijana wawili wa kipalastina ,mmoja akiwa na umri wa miaka 20 na wa pili 23 waliuliwa.
Waisrael wananunua silaha kwa wingi
Kutokana na wimbi hili linalotisha la mashambulio yasiyokuwa na dalili ya kusita,Israel imetangaza hatua kali za ziada ikiwa ni pamoja na ile ya kupunguza makali ya sheria ya watu kumiliki silaha.Gazeti linalosomwa na wengi nchini Israel limejaa picha za wayahudi wanaonunua vibomba vya gesi za kutoa machozi,marungu huku wanaouza bunduki wakisema mahitaji yameongezeka sana.
Huku hofu na wasi wasi ukiongezeka tangu majumbani mpaka majiani, wanajeshi wameshatawanywa katika mji wa kaskazini wa Haifa ambako wakaazi wanasemekana walimuona mtu mmoja na kuanza kupiga makelele wakisema ni gaidi.Mwanajeshi mmoja alifyetua risasi hewani na umati wa watu kutawanyika lakini hakuna gaidi yoyote mtuhumiwa aliyeshuhudiwa.
"Hili kweli ni wimbi la vitisho" amesema waziri wa ulinzi wa Israel Moshe Yaalon kupitia radio ya kijeshi,akizungumzia jinsi wananchi wenyewe walivyo mstari wa mbele,bila ya hofu na kufika hadi ya kubeba silaha.
Marekani yapanga kuwakutanisha Netanyahu na Abbas nchini Jordan
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anashinikizwa achukue hatua za kukomesha matumizi ya nguvu,lakini vijana wa kipalastina waliokata tamaa wanaonyesha hawajali.
Washambuliaji wanaonyesha hawafuati amri kutoka kwa mtu au shirika lolote-na kwa namna hiyo wanageuka kuwa changamoto kwa vikosi vya usalama ambavyo havijui nani ndie mwasisi anaestahiki kuandamwa .
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anapanga kulitembelea eneo hilo hivi karibuni.Anataraji kuwakutanisha kwa mazungumzo nchini Jordan,waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu