Raia Sudan Kusini wafariki bila idadi yao kamili kujulikana
11 Machi 2016Wanaume wanawake na watoto wameuwawa kwa kupigwa risasi, kuchomwa mishale, kuchomwa moto, kunyongwa, kukanyagwa kwa magari, kuzamishwa majini, kuachwa bila chakula hadi kufa, kuripuliwa na miili yao kuachwa mahali itakapoangukia au kufukiwa katika kaburi la pamoja.
Mwaka mmoja wakati wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Novemba mwaka 2014, shirika la kimataifa la kushughulikia mizozo ICG, linaloangalia hali ilivyo kwa karibu nchini humo, limeliambia shirika la habari la AFP kwamba watu takriban 50,000 waliuwawa. Mwaka huu Umoja wa Mataifa nao ukatoa idadi yake sawa na hiyo lakini baada ya muda wa miaka miwili.
Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya Sudan Eric Reeves, ambaye ni Profesa katika chuo kimoja nchini Marekani, amesema kushindwa kuhesabiwa vifo vilivyotokea ni ukosefu mkubwa wa maadili na kwamba hiyo huenda ikamaanisha maisha ya watu wa eneo hilo hayatiliwi maanani au hayaonekani kuwa na umuhimu.
Kwa upande wao wafanyakazi wa kutoa misadaa ya kiutu ambao hawakutaka kujulikana wanasema idadi ya waliyofariki huenda ikawa juu zaidi na kufikia watu laki tatu, idadi ambayo inafanananishwa na watu waliyofariki nchini Syria katika vita vinavyoingia mwaka wake wa tano.
Wachambuzi watoa maoni yao juu ya mauaji yanayosahaulika Sudan Kusini
Vifo hivyo vya Sudan Kusini vinajumuisha mauaji yaliyotokana na njaa kufuatia misaada ya kibinaadamu kuzuwiwa kufika maeneo ya waathirika, kama vile watu 40,000 ambao Umoja wa Mataifa ulionya kuwa wapo katika hali mbaya kufuatia maeneo yao kuwa hatari kufikia ili kuangazia pia hali ilivyo ikiwemo visa vya kikatili kama watu kufungiwa katika mapipa hadi kufa.
Vile vile vifo hivyo pia vinajumuisha wale waliyoangamia kutokana na ukosefu wa huduma za matibabu kufuatia kushambuliwa hospitali kadhaa katika eneo hilo. Madaktari wasio na mipaka MSF wameonya kuwa huenda kukatokea madhara mengine mengine zaidi kufuatia hospitali zake sita pamoja na Kliniki kushambuliwa kuvamiwa na kuchomwa moto mara kwa mara.
Aidha wachambuzi wanasema kushindwa kudhibitisha vifo vilivyotokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe inachangia mateso ya Sudan Kusini kukaa nje ya ramani ya kimataifa na kusababisha wanaotenda makosa hayo kukosa kuadhibiwa.
Lakini huku mapigano yakiendelea licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofanyika mwezi Agosti ushahidi wa wale waliyouwawa unaendelea kupotea. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, lililorekodi makaburi ya halaiki katika mji wa mashariki wa Bor mwezi wa Januari mwaka 2014 limeonya kuwa ushahidi unaendelea pole pole kupotea kutokana na makaburi yaliyofichika.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel