Hali kinu cha nyuklia cha Kursk bado mbaya - Grossi
24 Septemba 2024Kwenye mahojiano yaliyochapishwa leo na shirika la habari la Urusi, RIA, Grossi amesema hali hiyo mbaya inatokana na kuwepo kwa harakati za kijeshi karibu na kinu hicho.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo ya shirika la atomiki la Umoja wa Mataifa amesema shirika lake halina mpango wa kuweka kikosi cha kudumu kwenye kinu hicho kama ambavyo limeweka kwenye vinu vyengine vinne nchini Ukraine, kikiwemo cha Zaporizhzhia kilichochukuliwa na jeshi la Urusi mwanzoni kabisa mwa uvamizi wake Februari 2022.
Soma zaidi: Urusi inasema raia 56 waliuawa wakati Ukraine ilipolishambulia eneo la Kursk
Vikosi vya jeshi la Ukraine bado vipo kwenye mkoa wa kusini mwa Urusi, Kursk, baada ya uvamizi wao wa mwezi uliopita, lakini vimeweka kambi umbali wa kilomita 40 kutoka kwenye kinu hicho cha nyuklia.