Hali Marekani "inatia wasiwasi mkubwa" - Mkuu wa Siemens
4 Juni 2020Akizungumza na mtangazaji wa televisheni ya DW Brian Thomas, Kaeser amesema aliishi Marekani kwa miaka sita, na anaipenda sana nchi hiyo. Lakini sasa ana wasiwasi kuhusu mambo yanayoendelea huko. Anatumai kuwa serikali na kila mmoja katika ngazi ya uongozi ataweza kuyadhibiti matukio hayo na kuruhusu maandamano ya amani. "Hii ni mojawapo ya madola makubwa duniani. Tumekuwa tukiitazama Hong Kong na tumekuwa na wasiwasi kuwa watu hawawezi kwenda mitaani na kuelezea maoni yao kwa amani. Sasa inaonekana kuwa tunaona hali kama hiyo katika mojawapo ya nchi maarufu na nzuri zaidi ulimwenguni."
Kaeser, ambaye anatazamiwa kuondoka kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Siemens ifikapo Februari 2021, pia anaona mgawanyiko unaoendelea kuongezeka baina ya Marekani na China kuwa mojawapo ya mambo yanayotia wasiwasi shughuli za kibiashara katika muda mfupi ujao. Ameonya wafuatiliaji kuwa juhudi au mchakato wa kuivunja minyororo ya usambazaji bidhaa na taratibu za kibiashara ambazo kwa miongo mingi zimedhihirisha uhusiano wa kiuchumi kati ya madola hayo mawili huenda ukaziwekea mbinyo kampuni nyingi.
Alipoulizwa kama kuna utofauti wa biashara, Kaeser alisema huenda upo. Lakini suala la msingi hapa ni tofauti. Na ni mapambano ya nani atakuwa dola kubwa la kiuchumi katika muongo ujao. Ameonya kuwa mataifa hayo yanahitaji kuamua kati ya rafiki na adui akiongeza kuwa njia pekee ya kuendelea ni kwa makampuni kuchukua njia tofauti na kuzianzisha biashara zao nchini Marekani na China.
Kama tu ilivyo kwa makampuni mengine mengi yanayoendesha operesheni zake kimataifa, Siemens imekabiliwa na changamoto ya kudumisha shughuli zake wakati wa mlipuko wa COVID-19, huku zikipungua kwa asilimia 9 mwaka hadi mwingine katika matokeo ya kifedha ya kampuni hiyo ya robo ya pili ya mwaka.
Uamuzi upo wazi kuhusu ni wapi ulimwengu unaelekea baada ya COVID-19. Lakini natumai kuwa ulimwengu umejifunza kitu kutokana na janga la corona. Maisha hayawezi kuendelea kama zamani. Tumeiumiza sana dunia. Tumeiwekea jamii mbinyo mkubwa. Amesema mkuu huyo wa kampuni ya Siemens.
Hata hivyo, mkuu huyo wa Siemens anaona fursa katika hatua mpya za Ujerumani za kuchochea uchumi, zilizowekwa kuukwamua uchumi kutokana na athari zinazoendelea za janga hilo. Washirika katika serikali ya mseto wanaujadili mpango wa hadi euro bilioni 100.
Kaeser anasema tunahitaji kuutengeneza mpango huo katika njia ambayo hautakuwa deni kubwa bali utakuwa ni fursa kwa ajili ya siku za usoni. Itakuwa ni fursa ya uwekezaji kama utatekelezwa vizuri. Ukiutengeneza vibaya, basi utafuata mkondo zilizojikuta baadhi ya nchi za Ulaya na kwingineko.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo