1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Pakistan

24 Agosti 2010

Uchumi wa Pakistan kupata pigo kubwa kufuatia mafuriko nchini humo.

https://p.dw.com/p/Ouh6
Maeno mengi bado yako chini ya maji Pakistan.Picha: AP

Rais wa Pakistan Ali Asif Zardari ameonya kuwa nchi hiyo itachukua takriban miaka mitatu kujikwamua kutokana na athari za mafuriko mabaya kabisa kuwahi kulikumba taifa hilo. Mamilioni ya watu waliathirika na mafuriko Pakistan, huku maeneo mengi bado yako chini ya maji.

Kulingana na taarifa katika vyombo vya habari Rais Zardari alinukuliwa akisema hana matumaini iwapo Pakistan itarejea katika hali yake kabla ya mafuriko hayo, lakini akasema kwa sasa watatia bidii kuendelea na maisha.

Pakistan / Flut / Hochwasser / Baby / NO-FLASH
Mamilioni ya watu wameathirika na mafuriko Pakistan.Picha: AP

Zardari alisema itachukua miaka mitatu kwa Pakistan kuweza kuhimili pigo iliopata kutokana na mafuriko hayo, yaliyoanza Julayi 28 na ambayo yameharibu vijiji vingi, barabaraza zimefurika maji huku miundo mbinu ikiharibika kutokana na mafuriko hayo.

Sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa Pakistan imepata pigo kubwa. Mafuriko hayo yaliharibu kiasi cha ekari milioni moja na laki saba za pamba, mahindi pamoja na mimea ya miwa. Akiba nyingi ya vyakula ikiwemo mtama pia ilizombwa na kuharibiwa na mafuriko hayo.

Inakisiwa kuwa ukuaji wa uchumi utalemaa kwa kiasi cha kati ya sufuri na asilia mia tatu, kinyume na ilivyobashiriwa kabla ya mafuriko hayo. Pakistan ilikuwa inataraji uchumi wake utakua kwa kiasi cha asili mia 4.

Maafisa wa fedha wamekuwa wakifanya mkutano na maafisa wa Shirika la fedha ulimwenguni IMF kutafakari upya deni la Pakistan la kiasi cha dola bilioni 10.  Serikali ya ya nchi hiyo pia imelaumiwa kwa kuzembea kukabiliana na hali Pakistan, hasa baada ya maji kuanza tena katika maeneo ya milima Kaskazini mwa nchi hiyo.

Pakistan / Flut / Hochwasser / Zeltlager
Wahanga Pakistan bado wanaishi katika makambi.Picha: AP

Baadhi ya waatalam wanasema wasiwasi ya uhaba wa chakula, pamoja na hali ngumu ya maisha huenda ikaibua hali ya vurugu nchini Pakistan na kulitia katika mzozo taifa hilo ambalo ni mshirika mkuu wa nchi za Magharibi.

Rais Zardari binafsi ameshtumiwa vikali kwa kuendelea na ziara yake nchini Ufaransa na Uingereza ilhali taifa lake lilikuwa katika hali mbaya ya mafuriko. Lakini rais huyo alijitetea akisema alikuwa na sababu nzuri ya kuweko alikokuwa wakati janga hilo lilipotokea na kwamba shutma dhidi yake zimemhakikishia kuwa watu wa Pakistan walimhitaji ndio maana walitaka awepo nchini humo wakati huo wa mafuriko.

Wakati huo huo, Shirika la fedha ulimwenguni IMF limesema Pakistan inakabiliwa na wakati mgumu kugawanya fedha walizonazo kuikarabati nchi hiyo baada ya janga hilo la mafuriko. Hata kabla ya kutokea kwa mafuriko, uchumi wa Pakistan kwa miaka miwili ulikuwa unakabiliwa na mgogoro mkubwa. Sasa serikali inakabiliwa na tatizo la kukabiliana na hali y akiutu nchini humo, uharibifu wa mimea pamoja na miundo mbinu na vile vile suala la kupungua kwa utoaji wa ushuru.

Mwandishi: Munira Muhammad/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman