Hali Pakistan
21 Februari 2008Viongozi wa vyama viwili vikuu vya Upinzani nchini Pakistan wanakutana jioni hii kwa mara ya kwanza tangu kumalizika uchaguzi wa bunge ambapo vyama hivyo vilipata ushindi mkubwa,ili kujadiliana juu ya kuunda serikali. Viongozi hao wa vyama vya Pakistan Peoples Party ( ppp ) na Muslim League N cha Nawaz Sharif wanatafuta wingi wa thuluthi mbili ya viti bungeni kuweza kumtoa madarakani rais Musharaf.Tayari chama cha PPP cha Marehemu Benazir Bhutto kimekubaliana kushirikiana na chama kidogo cha Awami. Wakati huohuo maelfu ya raia wapakistan wamejitokeza katika maandamano ya kumpinga rais Musharraf.
Asif Ali Zardari kiongozi wa chama cha Pakistan Peoples Party na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif wanajadiliana jioni hii juu ya kuunda muungano ambao unaweza ukachangia katika kumuondoa madarakani rais Pervez Musharraf kufuatia kushindwa chama chake katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jumatatu iliyopita.
Vyama vingine vidogo tayari vinasimama katika upande wao hii ikiwa na maana kwamba vyama hivyo vinakaribia kupata wingi wa thuluthi tatu ambao unahitajika kumuondoa madarakani rais Musharaf.
Mkutano huo wa leo baina ya wanasiasa hao waupinzani yanafanyika huku polisi wakifyatua gesi za kutoa machozi katika mji wa Karachi dhidi ya maandamano ya mawakili wanaotaka arudishwe kazini jaji mkuu ambapo mawakili tisa wamekamatwa na wengine watatu wakajeruhiwa vibaya kwenye mapambano hayo.Maandamano ya wananchi dhidi ya Musharraf pia yamefanyika katika miji mbali mbali ya nchi hiyo.Kwenye mji wa lahore kiasi cha wanasheria 2000 wameandamana huku wakiimba nyimbo za kumtaka rais Musharaf ang'atuke mamlakani.Mawakili hao wanamtaka rais Musharraf amrudishe kazini jaji Mohammed Cahudhry ambaye yuko chini ya kifungo cha nyumbani tangu kutangazwa kwa hali ya hatari na rais Musharraf ambayo imeshaondolewa.Kabla ya kuanza mkutano na kiongozi wa chama cha PPP Waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif aliijiunga na waandamanji na kuwahutubia mawakili waliokuwa wanaandamana nje ya nyumba ya jaji mkuu akisema utawala wa rais Musharraf si halali na unakwenda kinyume na katiba ya nchi.Mojawapo ya masuala muhimu ya kujadiliwa katika harakati za kuunda muungano ni kumrudisha kazini jaji mkuu ambaye atakuwa katika nafasi nzuri ya kuubatilisha ushindi wa rais Musharraf unaotiliwa shakashaka.
Mapema leo hii kiongozi wa chama cha PPP Asif Ali Zardar alikutana na kiongozi wa chama kidogo cha kabila la Pashtun cha Awami National Party ANP kilichopata ushindi dhidi ya vyama vingine vya waislamu wenye itikadi kali katika eneo tete la kaskazini magharibi na kukubaliana kushirikiana kwa ajili ya maslahi ya nchi pamoja na demokrasia.
Hadi sasa lakini rais Musharraf ameshikilia msimamo wake kwamba hatajiuzulu kwa sababu amechaguliwa kisheria.Musharaf anaungwa mkono na Marekani kama mshirika wake dhidi ya mtandao wa kigaidi unaoongozwa na Osama Bin laden.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Musharraf atakachokifanya kwa sasa ni kujaribu kuwagawanya wapinzani wake yaani Zardari na Sharif na kumshawishi Zardari wa chama cha PPP ambacho kimeshinda viti vingi zaidi bungeni kuliko chama kingine kuunda mseto na chama chake cha muungano.
►◄