Hali ya hatari nchini Pakistan
5 Novemba 2007Yaliyokisiwa sasa yamethibitishwa.Kwani tangu miezi kadhaa kulivuma kuwa hali ya hatari itatangazwa ikiwa Rais Musharraf atajikuta mashakani.Tangu mwezi wa Machi Musharraf anapambana na Mahakama Kuu katika kinyanganyiro cha madaraka.Yeye alimfukuza kazi Jaji Mkuu wa Pakistan na baadae hakuwa na budi isipokuwa kukubali uamuzi wa Mahakamu kumrejesha kazini jaji huyo.
Uvumi wa vitisho vya kutangazwa hali ya hatari ulipokuwa ukienea,Musharraf alifanya kana kwamba anatekeleza mwito wa Marekani kuleta demokrasia nchini Pakistan.
Lakini siku chache zilizopita uvumi ulizuka upya. Kwani uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa ukingojewa iwapo kuteuliwa kwa Musharraf hapo mwezi wa Oktoba ni halali au la.Vitisho vya kutangaza hali ya hatari vilipaswa kuwashinikiza majaji kumuunga mkono Musharraf.Lakini yadhihirika kuwa siku chache kabla ya Mahakama kupitisha uamuzi wake, Rais Musharraf ameingiwa na hofu.Labda alipata fununu kuwa uamuzi utapinga kuteuliwa kwake.Au hakuweza tena kustahmilia hali ya kutegemea mahakama.
Lakini safari hii,Jemadari Musharraf amekwenda kombo kwani karata yake turufu ya mwisho,haina nguvu.Kutakuwepo upinzani mkali dhidi yake-kwanza kutoka kwa majaji,wanasheria na vyombo vya habari ambavyo hawezi kuvifunga tu kwa daima. Anavilazimisha vyama vya kisiasa,ikiwa ni pamoja na chama cha Benazir Bhutto cha PPP,kuchukua msimamo wa upinzani.Muda si muda hata udhia wa umma hautoweza kudhibitiwa.
Rais Musharraf,amehatarisha hadhi yake,kwani bado anaheshimiwa na Wapakistani wengi.Bila shaka amefanikisha mambo fulani kwa Pakistan-kama vile kupatana na India,uhuru wa vyombo vya habari na kwa jumla uhuru katika jamii pamoja na maendeleo ya kiuchumi.
Rais Musharraf atatazamia kuwa nchi za magharibi au angalao Marekani,zitamchukulia hata ikiwa hazipendelei kufanya hivyo.Hapo anatumia ujanja wa zamani unaofanya kazi tangu Septemba 11.Yaani majeshi ya Pakistan yanapigana vikali na wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu.
Wakati huo huo kuna sababu ya kudhania kuwa serikali mara nyingine hufumba macho,wanamgambo wanapojikusanya na kujipatia silaha.Ama vipi vikosi vya serikali vilikuta mrundiko wa silaha kwenye Msikiti Mwekundu kati kati ya Islamabad na mbele ya macho ya makachero
Kwanza michezo miwili ya Musharraf yapasa kuuzindia ulimwengu kuwa ni kweli kwamba hatari ya wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu ni kubwa–pili jeshi ni kinga pekee inayoweza kutegemewa kuwazuia Waislamu wa itikadi kali kunyakua madaraka.
Nchi za magharibi zinapaswa kujitenga na Musharraf.Ni kosa na hatari kudanganywa tena. Kwani hiyo miongoni mwa umma itachochea hisia za upinzani dhidi ya Marekani na nchi za Magharibi. Hata vyama vya kidini vitajitokeza kama upinzani wa kidemokrasia,ikiwa Musharraf hatobadili kauli yake haraka.
Sasa ni wakati wa kuunga mkono makundi ya wastani yaliyoimarika katika sekta ya sheria,vyombo vya habari,jumuiya ya kiraia pamoja na vyama vya kisiasa.Pakistan yenye demokrasia ndio itakyoweza kuwashinda wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu.