1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hatari yatangazwa jimbo la Missouri

Josephat Nyiro Charo18 Novemba 2014

Gavana wa jimbo la Missouri nchini Marekani Jay Nixon ametangaza hali ya hatari jimboni humo Jumatatu (17.11.2014) huku jopo maalumu la majaji likijiandaa kupitisha uamuzi kuhusu mauaji ya kijana mweusi wa Kimarekani.

https://p.dw.com/p/1Dp2D
USA Missouri Gouverneur Jay Nixon
Gavana wa jimbo la Missouri Jay NixonPicha: Scott Olson/Getty Images

Akitangaza hali ya hatari jimboni Missouri gavana Nixon pia ameliamuru jeshi la jimbo hilo liisaidie polisi iwapo kutatokea machafuko kama jopo la majaji litaamua limfungulie kesi au lisipate ushahidi wa kutosha kumfungulia mshitaka afisa wa polisi Darren Wilson aliyempiga risasi na kumuua kijana Mmarekeni mweusi Michael Brown aliyekuwa na umri wa miaka 18 mnamo Agosti 9 mwaka huu.

Gavana Nixon pia ameipa mamlaka idara ya polisi ya kaunti ya St Louis kusimamia maandamano yatakayotokea badala ya polisi ya Ferguson, Missouri. Meya wa mji wa St Louis Francis G Slay amesema anaunga mkono uamuzi wa gavana Nixon kuiruhusu polisi ya St Louis iwe na jukumu la kuwalinda waandamanaji kwa sababu anahisi wanaufahamu vyema mji huo pamoja na wakaazi wake na mafunzo waliyoyapata yanafaa zaidi kwa hali yoyote inayoweza kujitokeza.

Wakaazi wa Ferguson, ambao walishuhudia wiki kadhaa za maandamano yaliyogubikwa na machafuko kufuatia mauaji ya Michael wanajiandaa kwa machafuko yanayoweza kutokea hususan kama majaji wataamua wasimfungulie mashtaka ya uhalifu afisa wa polisi wa Ferguson aliyemuua kijana huyo.

Meya wa St. Louis Francis G. Slay (kushoto)
Meya wa St. Louis Francis G. Slay (kushoto)Picha: M. Muratovic

Meya Slay amesema hafahamu ni wanajeshi wangapi watakaotumwa St Louis na lini watakapotumwa, lakini anaamini wanaweza kwenda wiki hii. Amesema kikosi cha wanajeshi kitatokea maeneo mbalimbali ya jimbo la Missouri. Baadhi yao wana uzoefu na utekezaji wa utawala wa sheria, lakini wengi wao hawana uzoefu wowote wa maandamano ya amani kama maafisa wa polisi.

"Tutajiandaa kama watekelezaji wa sheria kuhakikisha watu na mali ziko salama pamoja na waandamanaji. Waandamanaji watakuwa na fursa ya kutumia haki zao kisheria kuandamana kwa njia ya amani. Wakati huo huo tunataka kuhakikisha tutakuwa na raslimali zinazohitajika iwapo kutatokea machafuko au kitu chochote kama hicho."

Maandamano yafanyika

Maandamano yamekuwa yakishuhudiwa kwa siku mbili sasa huko Ferguson huku ripoti ya jopo la majaji ikisubiriwa. Watu kadhaa waliandamana jana katika barabara za mji wa Clayton, Missouri, ambako jopo hilo linakutana.

Mama huyu ambaye hakujitambulisha alikuwa miongoni mwa waandamanaji. "Hivi ndivyo demokrasia ilivyo. Unatakiwa kwenda kokote unakoweza kuwasilisha ujumbe wako."

Michael Brown Zeichnung Ferguson USA
Michael Brown wakati wa uhai wakePicha: picture-alliance/AP Photo

Maafisa wamesema uamuzi unaweza kutolewa siku yoyote mwezi huu. Baadhi ya shule zimejulisha wazazi zitawaruhusu wanafunzi warejee nyumbani mapema wakati uamuzi huo utakapotolewa na biashara nyingi karibu na eneo lililoshuhudia machafuko mabaya kabisa baada ya mauaji ya Brown, zimeziba madirisha yao kama hatua ya tahadhari.

Kumekuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu kilichotokea wakati wa tukio la kupigwa risasi kijana Brown huku baadhi ya mashahidi wakisema alikuwa ameinua mikono yake kujisalimisha wakati alipopigwa risasi na wengine wakielezea kuhusu makabiliano kati yake na afisa Wilson.

Waandamanaji wengi waliingiwa na ghadhabu mwishoni mwa juma lililopita waliposikia afisa huyo huenda akarejea kazini kama hatatiwa hatiani, ingawa polisi ilisema atafutwa kazi mara moja kama atafunguliwa mashitaka.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman