Hali ya Kisiasa Pakistan
13 Machi 2009Mawakili na chama upinzani kinachoongozwa na Nawaz Sharrif wamekuwa mstari wa mbele kuandaa maandamano hayo kuishurutisha serikali ya Zardari kuwarejesha kazini majaji zaid ya 60 waliotimuliwa na utawala wa kijeshi uliopita wa Pervez Musharraf.
Kwa siku ya pili leo, polisi katika majimbo kadhaa nchini Pakistan wameendelea kuweka vizuizi kuzuia safari ya waandamanaji hadi katika mji mkuu wa Islamabad- kumtaka rais Asif Zardari awarejeshe kazini majaji wa mahakama kuu waliofukuzwa kazi na rais Pervez Musharraf alipotangaza hali ya hatari mwaka wa 2007.
Zaidi ya watu 750 wametiwa nguvuni hadi kufikia leo, huku mkoa wa Punjab wenye msisimko mkuu wa kisiasa ukiwa ndio ulioathirika zaidi. Mapema leo polisi walimzuia Ali Ahmed Kurd, rais wa chama cha mawakili, aliye na makaazi yake Lahore, kufunga safari yeye na wenzake kuelekea Islamabad.
Hata hivyo, wameapa watafika Islamabad kwa njia yeyote ile....
Jana ilikuwa zamu ya Karachi pale mamia ya waandamanaji walikamatwa walipokuwa safarini kuelekea Islamabad...Hali imekuwa si tulivu Pakistan, huku dola za Magharibi ambazo ni washirika wakuu wa Pakistan katika vita dhidi ya Wataliban na mirengo yenye siasa kali wakiingiwa na wasiwasi.
Wanadiplomasia kutoka Marekani na Uingereza na mataifa kadhaa wamekuwa wakijaribu kuuzima mgogoru huu kwa mazungumzo kati ya vyama hasimu, kile cha Pakistan Muslim league kinachoongozwa na Nawaz Sharrif na Pakistan People Party cha rais Asif Zardari.
Mawakili wanaongoza maandamano hayo wanamshtumu Zardari kwa kukiuka ahadi aliyotoa kuwa atawarejesha kazini majaji waliotimuliwa, punde tu atakapoingia madarakani- mwaka sasa, na rais Zardari amekuwa kimya.
Mjumbe maalum wa Marekani nchini Afghanistan, Richard Hoolbroke, na balozi wa Marekani nchini Pakistan, Anne Paterson, jana walizungumza na Zardari kujaribu kupata suluhu ya mzozo huu wa kisiasa.Pia walizungumza na kiongozi wa upinzani Nawaz Sharrif.
Wakati huo huo, wapiganaji 24 wa kitaliban wanasemekana wameuawa baada ya kombora la wanajeshi wa Marekani kutupwa katika mji wa Kurram huko huko Pakistan ulio mpakani na Afghanistan.
Wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa kitaliban katika majimbo yalio mpakani mwa Pakistan na Afhghanistan. Mashambulizi ya makombora ya Marekani yamewaua zaid ya wapiganaji 330 wa Kitaliban tangu kuingia madarakani rais Asif Zardari, aliye mshirika mkuu wa Marekani.
Mwandishi:Munira Muhammad/ AFP
Mhariri:Othman