Hali ya mashaka yaendelea Marekani
16 Oktoba 2013Wawakilishi wa vyama vya Republican na Demokratik walikutana kwa mara nyingine katika juhudi za kuutatua mgogoro wa bajeti unaoikabili Maerkani. Lengo la mazungumzo hayo lilikuwa kutafuta mwafaka juu ya kuiepusha serikali ya Marekani kuwamo katika hali ya kutokuwa na uwezo wa kutimiza dhima zake za kifedha.
Mazungumzo hayo yalisambaratika. Sasa serikali ya Marekani imebakiwa na muda usiozidi saa 24 ili kuweza kuiepesha hali hiyo. Ikiwa wajumbe wa vyama vya Republican na Demokratik hawatakubaliana juu ya kuiruhusu serikali kuongeza deni,serikali hiyo haitakuwa na uwezo wa kifedha wa kuzilipia gharama zake.
Obama ataka mapatano
Rais Barack Obama ametoa mwito wa kufikiwa mapatano mnamo wiki hii. Amesema ikiwa hatua haitapigwa haraka kwenye Baraza la Seneti na kwenye Baraza la wawakilishi,na ikiwa Republican hawana dhamira ya kuyaweka kando baadhi ya matashi yao ya kiitikadi kwa manufaa ya nchi, basi inawezekana ,serikali ikaingia katika hali ya kutokuwa na uwezo wa kulipia gharama zake.
Baadaa ya mazungumzo ya hapo jana kusambaratika, vyombo vya habari vimeripoti kwamba sasa wajumbe wa Baraza la Seneti wamelichukua jukumu la kufanya mazungumzo. Rais Obama amesema mazungumzo yaliyofanyika hapo jana yalikuwa vurumai tupu. Hata hivyo amesema anatumai suluhisho litafikiwa kabla ya hapo kesho alhamisi, yaani siku ambapo serikali ya Marekani inaweza kuanza kuwa muflisi ikiwa haitaruhusiwa kuendelea kukopa.
Wakati huo huo shirika la, Fitch linalopima uwezo wa nchi wa kulipa madeni limetahadharisha juu ya uwezekano wa kuishusha hadhi ya Marekani kutoka kwenye alama za AAA zinazoashiria uwezo wa juu kabisa wa nchi wa kuzitimiza dhima zake za kifedha.
Matumaini bado yapo
Viongozi wa Baraza la Seneti pia wamesema wanatumai suluhisho litafikiwa,katika dakika za mwisho baina ya wawakilishi wa vyama vya Republican na Demokratik ili kuumaliza mkwamo wa bajeti. Kutokana na uhaba wa muda,na kutokana na shinikizo la masoko na mtazamo wa wananchi, kiongozi wa Demokratik katika Baraza la Seneti, linalodhibitiwa na chama chake, Harry Reid na kiongozi wa maseneta wa chama cha Republican ambao ni wachache katika baraza hilo, Mitch McConnell wanatumai kufikia mapatano na kupeana mikono yumkini baadae leo.
Wataalamu wa uchumi wametahadharisha juu ya madhara yanayoweza kutokea katika uchumi wa Marekani na wa dunia nzima ikiwa Marekani haitautatua mgogoro wa bajeti hadi kufikia hapo kesho alhamisi.
Mwandishi:Mtullya Abdu./afp,rtre
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman