1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas, jeshi la Israel wapambana kusini mwa Gaza

6 Desemba 2023

Wanajeshi wa Israel wanaendelea kukabiliana na wanamgambo wa Hamas kwenye Ukanda wa Gaza baada ya kutanua operesheni ya mashambulizi ya ardhini hadi mji wa pili kwa ukubwa kusini mwa ukanda huo.

https://p.dw.com/p/4Zpd3
Gazastreifen Israel Krieg mit Hamas
Hali ilivyo wakati wa mashambulizi ya Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya tarehe 6 Disemba 2023.Picha: Jack Guez/AFP

Hatua hiyo inaendelea kulipunguza kabisa eneo ambalo Wapalestina wanaweza kutafuta hifadhi na kusitisha usambazaji wa msaada muhimu katika maeneo mengi ya ukanda huo. 

Mashambulizi ya upande wa kusini yanatishia kuhama zaidi kwa watu katika eneo hilo la pwani lililozingirwa, ambako Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 1.87, tayari wameyakimbia makaazi yao.

Soma zaidi: Mapigano makali yaendelea Ukanda wa Gaza

Jeshi la Israel limesema jana kuwa wanajeshi wake wako katikati ya mji wa kusini wa Khan Younis baada ya kile ilichoelezea kuwa ni "siku ya mashambulizi makali zaidi" tangu kuanza kwa operesheni hiyo ya ardhini wiki tano zilizopita, huku kukiwa na mapambano makali pia katika upande wa kaskazini. 

Awali Israel ilikuwa imewataka wakaazi wa Gaza walioko upande wa kaskazini kukimbilia upande wa kusini kujilinda na mashambulizi yake ya anga.