1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburg yaendelea kukaza kamba

13 Machi 2017

SV Hamburg, imeyapiga jeki matumaini yao ya kubakia katika ligi kuu ya Bundesliga baada ya kutoka nyuma na kupata ushindi mgumu kweli wa mabao 2-1 dhidi ya Borussia Moenchengladbach

https://p.dw.com/p/2Z6nJ
Bundesliga Hamburger SV v Borussia Moenchengladbach Bobby Wood
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Rose

Hamburg ambayo haijawahi kushushushwa ngazi katika Bundesliga, inabakia katika eneo la kuchezwa mechi za mchujo kwa tofauti ya mabao nyuma ya Wolfsburg na Werder Bremen lakini imeikaribia Augsburg na pengo la pointi mbili tu.

Jonas Hofmann, ni mchezaji wa Borussia Mönchengladbach na hapa anazungumzia kichapo chao "Bila shaka nasi pia tulitaka kushinda lakini nadhani hamburg waliutafuta ushindi zaidi yetu uwanjani. Hatukuweza kujituma vizuri na wakati mwingine tulikuwa na muda mfupi sana. Tunaenda nyumbani bila pointi yoyote na hatuwezi kulalamika".

Schalke ilipata ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Augsburg na kupata angalau mwanya wa kupumua katika Bundesliga. Ushindi huo uliwasogeza katika nafasi ya 11 na kocha Markus Weinzierl aliwasifu vijana wake "Tuliendelea pale tuliachia Alhamisi iliyopita, na tumecheza kwa kujituma katika kipindi cha kwanza na kufunga 3-0. Katika kipindi cha pili, tuligundua kuwa tunaongoza kwa 3-0 na hivyo kulegea. Tulikosa bao la nne katika counter attack lakini kwa jumla ni ushindi uliostahiki"

Bundesliga 24. Spieltag RB Leipzig gegen VfL Wolfsburg
Wolfsburg waliwaduwaza Leipzig Picha: Getty Images/Bongarts/M. Kern

Kileleni mwa ligi hakuna mabadiliko yoyote baada ya Bayern Munich kuilaza Eintracht Frankfurt 3-0 siku ya Jumamosi. 

Ni matokeo ambayo yameipa Bayern uongozi wa pengo la pointi 10 dhidi ya nambari mbili RB Leipzig.  Manuel Neuer ni mlinda mlango wa Bayern "Kwanza lazima tuseme Frankfurt wakikuwa wakakamavu na wakali katika mashambulizi na tulikuwa na matatizo mwanzoni. Tulipoteza umakini hapa na pale hasa katika kupeana pasi katika mfumo wetu na kuwaruhusu Frankfurt kupata nafasi nyingi za kufunga mabao maana tuliwaruhusu tena na tena. Bahati nzuri tuliimarika katika mchezo na kupata matokeo mazuri katika kipindi cha pili".

Leipzig walinyamazishwa nyumbani 1-0 dhidi ya Wolfsburg wakati kukiwa na mechi 10 zilizosalia kwa msimu kukamilika. Kocha Ralph Hasenhüttl alisema hawakutumia nafasi zao vyema "Tulikuwa na nafasi kadhaa nzuri za kufunga bao. Lakini kawaida ilikuwa kazi kweli. Mara kadhaa hatukufanya maamuzi muhimu katika mchezo. Na kama utafungwa bao basi inakuwa vigumu kurudi katika mchezo. Tuligundua kuwa hatukuwa na kasi sana hasa wakati tuliopoteza mpira uwanjani. Tulifanya makosa mengi sana na tukashindwa kufunga mabao kutokana na nafasi nyingi".

Fussball Bundesliga 24.Spieltag - Borussia Dortmund vs Hertha Berlin
BVB wanashikilia nafasi ya tatu licha ya kichapoPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Hertha Berlin walikwamilia nafasi ya tatu na kuuwekea kikomo ushindi wa mechi nne mfululizo wa Borussia Dortmund wanaoshikilia nafasi ya tatu baada ya kuwafunga 2-1. Msikilize Thomas Tuchel "Inakera, tungeepusha hilo. Ni kitu tulijitakia wenyewe. Hakika tulikuwa na nafasi nzuri za kuwa kifua mbele katika mchezo, lakini tukafanya makosa makubwa ya mtu binafsi na tukajikuta nyuma. Hatukuwa na shuti nyingi kuelekea lango la adui na matokeo yake ni kuwa tulikosa kutumia vyema nafasi na kuwa makini katika lango la adui ili kupata usnindi".

Katika matokeo mengine, washika mkia Darmstadt waliandika ushindi wao wa nne msimu huu kwa kuwafunga Mainz 2-1. Hoffenheim ilitoka sare ya 1-1 na Freiburg 1-1 na kubakia katika nafasi ya nne ambayo ni tikiti ya mwisho ya kandanda la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Cologne ilitoka sare ya 2-2 na Ingolstadt inayokabiliwa na kitisho cha kushushwa ngazi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga