1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hannover 96 kinadharia imeshuka daraja

Admin.WagnerD25 Aprili 2016

Hannover 96 yashuka daraja, lakini homa bado iko juu kwa majina makubwa ya soka la Ujerumani , Eintracht Frankfurt , Werder Bremen na VFB Stuttgart zinakabiliwa na wakati mgumu katika kuepuka kushuka daraja.

https://p.dw.com/p/1IcOf
Bundesliga Eintracht Frankfurt gegen FSV Mainz 05
Wachezaji wa Eintracht Frankfurt wakishangiria bao la ushindi dhidi ya Mainz 05Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Hannover 96 huenda imeliaga daraja la juu katika Bundesliga lakini majina makubwa katika soka la Ujerumani kama Eintracht Frankfurt , Werder Bremen na VFB Stuttgart zinakabiliwa na michezo migumu katika juhudi zao za kuweka matumaini hai ya kubakia katika daraja la juu.

Eintracht Frankfurt iliishjinda Mainz 05 jana Jumapili kwa bao la dakika za mwisho na vilio vya hofu vilisikika kwa mashabiki wa Bremen na Stuttgart.

Bundesliga Borussia Mönchengladbach - 1899 Hoffenheim
Wachezaji wa Borussia MoenchengladbachPicha: picture alliance/dpa/M. Becker

Wakati maisha katika ligi daraja la pili yamekwisha amuliwa , timu inayokamata nafasi ya pili kutoka mwisho Frankfurt ina pointi 30 moja tu nyuma ya Werder Bremen iliyoko nafasi ya tatu kutoka mwisho,wakati VFB Stuttgart kwa sasa iko salama, lakini ni kwa sasa tu kwani ina pointi 33.

Hoffenheim iko katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 34 lakini imebadilika kwa kiasi kikubwa chini ya kocha kijana Julian Nagelsmann na Darmstadt iliyopanda daraja msimu huu ikiifuatia ikiwa na pointi 35, kwa wakati huu timu hizo zina nafasi kidogo ya kupumua.

Hali hii inaziweka Eintracht Frankfurt, VFB Stuttgart na Werder Bremen , klabu tatu zenye historia ndefu katika bundesliga zikiwa zimeshanyakua taji la ubingwa wa ligi baina yao, ziko katika kitisho kikubwa cha kushuka daraja.

Huyu hapa mchezaji wa Eintracht Frankfurt Marco Russ.

"Kama ilivyoonekana kwa mashabiki wetu kwa mara nyingine , katika wakati huu mgumu sana wakiwa pamoja na kuanzia mwanzo hadi mwisho wakituunga mkono ,inakuwa rahisi kwetu kupambana katika mchezo. Nafikiri kwa jinsi tulivyocheza tumewaonesha mashabiki wetu , kwamba bado hatujafa , na kila kitu bado kiko wazi. Itakuwa vigumu, lakini hatukati tamaa."

Bundesliga VfB Stuttgart vs Borussia Dortmund Christian Pulisic
Christian Pulisic akishangiria bao alilofunga dhidi ya StuttgartPicha: imago/T. Bielefeld

Bayern Karibu na ubingwa

Bayern Munich imesogea karibu na ubingwa wake wa nne mfulilizo kwa kupungukiwa na pointi moja tu wiki hii baada ya kuishinda Hertha Berlin kwa mabao 2-0 na kuendeleza mwanya wa pointi saba dhidi ya Borussia Dortmund wakati ikisalia michezo mitatu Bundesliga kufikia mwisho.

Kikosi cha kocha nyota Pep Guardiola kinachosaka mataji matatu msimu huu kutoka jimbo la Bavaria hakifikia kiwango chake cha juu mchezoni siku ya Jumamosi lakini bado walifanikiwa kupachika mabao hayo mawili kupitia Arturo Vidal na Douglas Costa.

Borussia Dortmund iliitumbukiza VFB Stuttgart katika hali ya sintofahamu na wasi wasi mkubwa wa kushuka daraja pale ilipoishindilia mabao 3-0 , huku Bayer Leverkusen ikiigaragaza Schalke 04 na kuivurugia fursa ya kucheza michuano ya Ulaya mwakani kwa kuikandika mabao 3-2.

Borussia Moenchengladbach ilijihakikishia nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kuchapa TSG Hoffenheim kwa mabao 3-1 jana Jumapili.

Mchezaji wa kati wa Gladbach Granit Xhaka amesema.

"Tulihisi mbinyo ni mkubwa baada ya kushindwa mara mbili dhidi ya Ingolstadt na Hannover, ambapo hakuna kilichokwenda vizuri katika michezo hiyo, na tulihitaji kuchukua hatua. Nahisi leo tumefanikiwa."

Leicester yakaribia kunyakua ubingwa

Nchini Uingereza Leicester City iliirarua Swansea City kwa mabao 4-0 jana Jumapili na kusogea karibu kabisa na ubingwa wao wa kwanza wa ligi ya Uingereza ikiwania pointi tano tu kuweza kufanikisha lengo hilo wakati kumebakia michezo mitatu msimu kumalizika.

Meneja wa Leicester City Claudio ranieri amewatia nguvu wachezaji wake kwa ajili ya mchezo muhimu dhidi ya Manchester United, lakini anaamini kwamba hakuna timu yake inachoweza kushindwa kutokana na uwezo wao wa kupambana na ari.

Fußball EM 2016 Qualifikation Griechenland Färöer
Kocha wa Leicester City Claudio RanieriPicha: AFP/Getty Images/A. Tzortzinis

Leicester ambayo iliokoka kushuka daraja msimu uliopita, imejiweka pointi nane juu ya msimamo wa ligi jana na wanahitaji pointi tano kutoka katika michezo yao mitatu ya mwisho kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo Tottenham Hotspurs inaweza kupunguza mwanya huo hadi pointi tano kwa kuishinda West Bromwich Albion leo Jumatatu(25.04.2016) , na Ranieri ameonya kwamba mbio za timu yake kuelekea ubingwa bado hazijakamilika.

Mahrez mchezaji bora Uingereza

Mshambuliaji wa pembeni wa Leicester City Riyad Mahrez kutoka Algeria amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka bara la Afrika jana kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka nchini Uingereza, kama alivyochaguliwa na wachezaji wenzake katika ligi.

Großbritannien Leicester City - Riyad Mahrez
Mchezaji Riyadh Mahrez wa Leicester City mchezaji bora wa mwaka UingerezaPicha: Reuters/J. Cairnduff

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 raia wa Algeria mzaliwa wa Ufaransa, alipokea tuzo hiyo katika sherehe zilizofanyika mjini London.

Nusu fainali za Champions League barani Ulaya zinaanza kesho Jumanne wakati Real Madrid, Bayern Munich na Atletico Madrid zikiwania kuimarisha hadhi yao katika kinyang'anyiro hicho wakati Machester City ina matumaini ya kujitumbukiza nayo katika kundi hilo la mafanikio.

Bayern ina miadi na Atletico Madrid mjini Madrid siku ya Jumatano , wakati Real Madrid iliyolinyakua taji hilo mara nyingi zaidi ikipambana na Manchester City kesho Jumanne.

Champions League

Kesho Jumanne Manchester City inaikaribisha , mabingwa mara 10 wa Champions League Real Madrid na siku ya Jumatano Bayern inasafiri kwenda Madrid kupambana na Atletico wakati kocha wa Bayern Pep Guardiola anawania kuingia katika fainali yake ya kwanza na kikosi hicho cha mabingwa wa Ujerumani.

Kinyume na mawazo ya wengi kwamba kucheza nyumbani mchezo wa mkondo wa pili ni fursa nzuri ya kushinda , hakuna timu wenyeji wa mchezo wa mkondo wa pili imefuzu kuingia fainali tangu mwaka 2011.

Deutschland Müller und Lewandowski Jubel
Thomas Mueller na Robert Lewandowski wote wa Bayern Munich wakishangiria baoPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Bayern hususan haingependa kuanzia ugenini kwa kuwa iliyaaga mashindano hayo katika awamu ya nusu fainali katika juhudi za Guardiola za kufikia fainali ya kombe hilo kila mara akiwa na Bayern. Yuko hivi sasa katika muhula wake wa tatu madarakani akiwa na bayern kabla ya kutimkia Manchester City msimu ujao.

Kombe la FA

Crystal palace imeingia katika fainali ya kombe la FA nchini Uingereza na kurejesha kumbukumbu ya fainali hiyo mwaka 1990 dhidi ya Manchester United baada ya jana kuishinda Watford kwa mabao 2-1.

Hapa Ujerumani Bayern Munich na Borussia Dortmund ndio zitaumana mjini Berlin tarehe 21 mwezi ujao kuwania taji la kombe la shirikisho , maarufu kama DFB Pokal, ama kombe la chama cha kandanda nchini Ujerumani DFB.

Na huko nchini Tanzania Dar Young Africans ya Dar es Salaam iliingia katika fainali ya kombe la FA nchini Tanzania kwa utata baada ya kuishinda Coastal Union ya Tanga kwa mabao 2-1 hali inayopingwa vikali na Coastal Union.

Azam nayo ya Dar es Salaam pia ilifanikiwa kuingia katika fainali hiyo kwa kuzaba Mwadui FC ya Shinyanga kwa bao 1-0. Mchezo kati ya Yanga na Coastal Union ulivunjika dakika 105 baada ya kipindi cha kwanza cha nyongeza, baada ya mwamuzi kuonekana ameumizwa kwa kitu kama jiwe wakati huo Yanga ikiongoza mabao 2-1.

Riadha

Bingwa wa dunia mwaka 2003 wa mbio za mita 5000 Eliud Kipchoge wa Kenya ametetea ubingwa wake na kuweka rekodi katika mbio za Marathon za mjini London jana Jumapili.

London Marathon Eliud Kipchoge 2016 Virgin Money London Marathon
Eliud Kipchoge mshindi wa mbio ndefe za Marathon za mjini LondonPicha: Reuters/P.Childs

Kipchoge alishinda kwa kutumia saa 2 dakika 03.05 na kuweka rekodi mpya ya mbio hizo kwa sekunde 55.

Na watayarishaji wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 mjini Tokyo Japan leo wametangaza nembo mpya karibu miezi nane baada ya nembo ya kwanza kufutwa kutokana na kashfa ya madai ya kuiga, lakini pia imekosolewa kwamba haina mvuto.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae, afpe , rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman