HANOI : Mkutano wa APEC waanza
18 Novemba 2006Viongozi mataifa 21 yaAsia na Pasifiki wameanza mkutano wa siku mbili mjini Hanoi Vietnam leo hii kwa kutofautiana juu ya namna ya kukabiliana na tishio la nuklea la Korea Kaskazini lakini inaonekana kukubaliana katika suala la kufufuwa mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani WTO juu ya maendeleo.
Kabla ya dhifa ya chakula cha mchana ya mkutano huo wa viongozi Rais George W .Bush wa Marekani ameshindwa kumshawishi Rais mwenzake wa Korea Kusini Roh Moo- hyun kubadili msimamo wake juu ya Mpango wa Usalama wa Kuzuwiya Kuenea kwa Silaha za Nuklea ambao unatowa wito kwa mataifa kuzidukiza na kukaguwa meli zinazoshukiwa kubeba zana kwa ajili ya kutengenezea silaha za nuklea.
Roh amelikataa ombi binafsi la Bush kujiunga na ukaguzi wa meli za Korea Kaskazini unaongozwa na Marekani ili kuizuwiya nchi hiyo isimiliki zana na silaha zaidi za nuklea kufuatia jaribio lake la bomu la nuklea mwezi uliopita.
Mkutano huo wa APEC wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki unatazamiwa kutawaliwa na suala la biashara ya dunia na mzozo huo wa nuklea wa Korea Kaskazini.