Hansi Flick kuwa kocha mpya wa Ujerumani
25 Mei 2021Kocha wa zamani wa klabu ya Bayern Munich Hansi Flick amesaini mkataba kuwa kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani Die Mannschaft baada ya mashindano ya EURO 2020. Taarifa hiyo imetolewa Jumanne na shirikisho la soka la Ujerumani, DFB.
Makubaliano hayo yatakuwa halali hadi baada ya mashindao ya EURO 2024 yanayotarajiwa kufanyika hapa Ujerumani.
"Utiaji saini umefanyika kwa haraka mno kiasi cha kushangaza, hata kwa kwa mimi, lakini nafurahi sana kuwa kocha wa timu ya taifa kuanzia msimu wa mapukutiko," alisema Flick.
Baada ya miezi 18 ya ufanisi katika klabu ya Bayern Munich, ambako alishinda mataji saba na timu hiyo, Flick mara moja alipendelewa kama mtu ambaye angeweza kuchukua nafasi ya kocha wa sasa Joachim Loew, ambaye ataachia ngazi baada ya mashindano ya EURO yanayoanza mwezi ujao wa Juni.
Flick anachukua nafasi ya kocha Loew ambaye alikuwa bosi wake waliposhinda kombe la dunia la kandanda mwaka 2014 nchini Brazil, akiwa kocha msaidizi.
Mechi ya kwanza ya Flick itakuwa ya kufuzu kwa kombe la dunia huko Lichtenstein mnamo Septemba 2, ikifuatiwa na mechi yake ya kwanza nyumbani dhidi ya Armenia Septemba 5 na pambano kali dhidi ya Iceland siku tatu baadaye.
(dpa)