Harris aihimiza Vietnam kuungana na Marekani kuikabila China
25 Agosti 2021Kamala harris amesema Marekani inahitaji kutafuta njia za kuishinikiza China kuendelea kuheshimu mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu sheria ya bahari. Makamu huyo wa rais wa Marekani ameyasema hayo leo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Vietnam Nguyen Xuan Phuc.
Kauli yake hiyo inaendeleza ukosoaji wake dhidi ya China. Wakati wa hotuba yake huko Singapore Jumanne asubuhi, Harris alisema madai ya Beijing kuhusu eneo linalozozaniwa la bahari ya kusini mwa China ni ya kulazimisha na ya vitisho.
''Tutafanya kazi kwa karibu na Vietnam kudumisha utaratibu wa kimataifa wa sheria, pamoja na uhuru wa kusafiri, suala ambalo tunalichukulia kwa uzito, na ikiwa ni pamoja na suala linalohusiana na Bahari ya kusini mwa China.''
China ilijibu tuhuma hizo kupitia shirika la habari la serikali, ikiishutumu Marekani kwa unafiki katika kujaribu kuzilazimisha na kuzitisha nchi za kanda hiyo katika mpango wake wa kuidhibiti China.
Vitisho vya China kwebnye bahari ya kusini mwa China
China inadai Bahari ya China Kusini kuwa eneo lake, licha ya nchi zingine kupinga madai hayo,ikiwemo Vietnam. Beijing imejenga visiwa bandia na kuweka vifaa vyenye uwezo wa kijeshi katika eneo hilo.
Harris alisema Marekani itatoa boti mpya ya walinda pwani kwa Vietnam kusaidia nchi hiyo kuhifadhi eneo lake la baharini. Vietnam tayari imepokea boti mbili za aina hiyo kutoka Marekani.
Washington ilitangaza itazidisha uhusiano wa nchi mbili kati ya mataifa haya mawili kwa kiwango cha kile kinachoitwa "mkakati wa ushirikiano''. Harris pia alimwambia Rais Phuc kuwa uhusiano huo kati ya nchi hizi mbili umetoka mbali katika robo ya karne iliopita.
Wakati wa ziara yake, Harris alizindua ofisi ya kikanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia ya Kituo cha Kudhibiti Magonjwa- CDC, huku Vietnam ikikabiliwa na wimbi baya zaidi la janga la covid-19.
Ziara hiyo ya harris itakayo malizika Alhamisi ni ya kwanza kwa makamu wa rais wa Marekani nchini Vietnam tangu kumalizika kwa vita vya Vietnam mwaka 1975.