1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hasira dhidi ya Zuma, mgogoro Gabon magazetini

9 Septemba 2016

Mgogoro unaofukuta ndani ya chama cha Afrika National Congress ANC, kitisho cha ugaidi katika eneo la Sahara, na mgogoro wa uchaguzi nchini Gabon ndiyo mada zilizopewa kipaumbele na magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika.

https://p.dw.com/p/1JzXK
Südafrika Proteste vor ANC Zentrale in Johannesburg
Picha: Reuters/S. Sibeko

Gazeti la Neues Deutschland lililoripoti juu ya wanaharakati kutoka makundi hasimu ya chama tawala nchini Afrika Kusini ANC, waliokabiliana nje ya makao makuu ya chama mjini Johannesburg siku ya Jumatatu, wakimulika mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho wakati ambapo shinikizo linazidi kwa rais Jacob Zuma.

Likiwa na kichwa cha habari kisemacho hasira dhidi ya Zuma, gazeti la Neues Deutschland liliandika kuwa mnyukano ndani ya chama ANC unachukuwa mwelekeo mbaya kila kukicha, hasa baada ya matokeo mabaya katika uchaguzi wa manispaa ambayo yanalaumiwa kwa uongozi wa Zuma pamoja na masaibu ya kiuchumi.

Kundi la waandamanaji wapatao 300 lilikuwa limetangaza nia ya kuyakalia makao makuu ya chama, lakini upande mwingine walikuwepo wafuasi wa ANC wakiwemo kutoka matawi ya wanawake, vijana na maveterani wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi ambao waliwazuwia waandamanaji hao kuingia makao makuu ya chama.

Maveterani wa vita vya ukombozi wa Afrika Kusini wakilinda ofisi za chama cha ANC dhidi ya waandamanaji wanaoshinikiza rais Jacob Zuma ajiuzulu.
Maveterani wa vita vya ukombozi wa Afrika Kusini wakilinda ofisi za chama cha ANC dhidi ya waandamanaji wanaoshinikiza rais Jacob Zuma ajiuzulu.Picha: Reuters/S. Sibeko

Miongoni mwa madai yao ni pamoja na kumtaka Zuma pamoja na uongozi wote wa chama waachie ngazi na pia akiuzulu nafasi ya urais kwa sababu wanamini hana jipya zaidi ya kuwa mzigo kwachama na kukikosesha ushindi katika uchaguzi.

Gazeti la Neues Deutschland lnamnukuu wanachama wanadamizi wa ANC aliesema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ENCA, kuwa hali hiyo inatokana na ukwlei kwamba demokraisa ya ndani ya ANC haifanyi kazi tena.

Hofu ya kuenea kwa ugaidi wa IS Burkina Faso

Gazeti za die tageszeitung limeripoti juu ya kitisho cha kuenea kwa ugaidi wa kundi la Dola la Kiislamu IS katika eneo la Sahara. Gazeti hilo linamulika hasa hofu ya mashambulizi kaskazini mwa Burkina Faso. Linasema ingawa nchi hiyo imechukuliwa mara zote maskini, lakini ilikuwa inajulikana kwa utulivu na usalama wake. Lakini matukio yanayotukia katika nchi jirani ya Mali yanazidi kuitisha Burkina Faso.

Gazeti hilo linatilia maanani mashambulizi yaliotokea wiki iliyopita katika mji wa Markoye katika mpaka wa pamoja kati ya Burkina Faso, Mali na Niger, ambamo watu wawili waliuawa akiwemo mwaname mwenye umri wa miaka70, na maafisa watatu wa forodha walijeruhiwa. Washambuliaji hao waliripotiwa kutorokea nchini Mali kwa kutumia pikipiki. Mtandao w ainternet wa shirika la habari la Mauritania, ulilitaja kundi la Dola la Kiislamu kuhusika na mashambulizi hayo.

Shambulio katika mji wa Markoye ndiyo la saba nchini Mali tangu Aprili 2015.Lakini mashambulizi yaliyopamba vichwa vya habari ni yale yaliotokea katikakati mwa mwezi Januari dhidi ya hoteli ya Splendid na pia katika mkahawa wa Cappucino katikakati mwa mji mkuu Ouagdougou, ambamo watu 30 waliuawa.

Hoteli ya Splendid mjini Ouagadougou ilishambuliwa na wapiganaji wa Kiislamu.
Hoteli ya Splendid mjini Ouagadougou ilishambuliwa na wapiganaji wa Kiislamu.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Lakini kwa miaka kadhaa imekuwa ikihofiwa kuwa mkoa wa kaskazini wa Oudalan, unakokutikana pia mji wa Markoye, unaweza kugeuka ngome ya magaidi kutokana na uduni wa miundombinu na ukosefu wa udhibiti wa mipaka.

Mgogoro wa uchaguzi Gabon

Gazeti la die Tageszeitung limeandika juu ya mgogoro unaitikisa Gabon baada ya ushindi wa kutatanisha wa rais wa nchi hiyo Ali Bongo katika uchaguzi wa Agosti 27. Gazeti hilo limeandika kwamba Rais Bongo aliepata ushindi wa asilimia 49.8 dhidi ya asilimia 48.2 ya mpianzani wake Jean Ping amejikuta katika malumbano na waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya, aliyowatuhumu kwa kumpendelea mpinzani wake.

Timu hiyo ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya iliunga mkono madai ya mgombea wa upinzani Jean Ping, kwamba matokeo ya kila kituo yachapishwe ili kuwezesha mchakato wa kupinga matokeo mahakamani. Ukosoaji huo wa Umoja wa Ulaya unaupa nguvu upinzani, katika imani yao kwamba walishinda uchaguzi. Jean Ping anaamini yeye rais mteule wa Gabon na aliitisha mgomo wa umma ili kumkwamisha Bongo. Waziri wa sheria na naibu waziri mkuu Serapin Moundounga aliamua kujiuzulu nafasi yake kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Mahasimu wa Gabon - Rais Ali Bongo na mpinzani wake Jean Ping
Mahasimu wa Gabon - Rais Ali Bongo na mpinzani wake Jean PingPicha: picture-alliance/dpa/E.Laurent/L.JinMan

Kifo cha Johan Botha

Mwanamuzi mashuhuri Johan Botha, amefariki Alhamis wiki hii akiwa na umri wa miaka 51. Gazeti la Süddeuteche Zeitung limeripoti juu ya kifo cha msanii huyo mzaliwa wa Afrika Kusini mwenye uraia wa Austria, likimtaja kuwa mmoja wa waimbaji mashuhuri wa miondoko ya opera, akimudu vilivyo uimbaji katika lugha za Kijerumani na Kitaliana. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alisema Botha atakumbukwa kwa sauti yake tulivu na imara, akimtaja pia kama balozi wa Afrika Kusini nje ya nchi.

Na kwa ripoti hiyo ya gazeti la Südedeutsche Zeitung nami ndiyo nazifunga kurasa za magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika mnamo Juma hili. Ulikuwa nami Iddi Ssessanga, hadi wakati na mara nyingine.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche zeitungen

Mhariri: Saumu Yusuf