Hatimaye Bobi Wine aelekea Marekani kwa matibabu
1 Septemba 2018Mwanamuziki maarufu wa Uganda aliyegeuka kuwa mwanasiasa na mbunge wa upinzani Bobi Wine, hatimaye ameweza kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Wakili wa mwanamuziki huyo amewaeleza waandishi wa habari wa shirika la AFP kwamba mwanamuziki huyo nyota wa mtindo wa Reggae Robert Kyagulanyi Ssentamu mwenye umri wa miaka 36 maarufu kwa jina la usanii Bobi Wine amekwenda nchini Marekani kutibiwa baada ya kudaiwa kuteswa na vikosi vya usalama alipokuwa kizuizini.
Bobi Wine alibakia katika hospitali ya serikali siku ya Ijumaa baada ya maafisa wa usalama kumkamata siku ya Alhamisi alipokuwa anataka kuondoka nchini Uganda kwenda nje kwa ajili ya matibabu hali iliyochochea upya maandamano.
Jaji mkuu wa Uganda Bart Katureebe aliukumbusha umma kuwa katiba ya Uganda inazuia mateso na kuwapa ujumbe walinda usalama, kwamba wakati wanakamata raia wa Uganda, wahakikishe wanazingatia kuwa raia hao ni wanadamu sio wanyama. Wakili wa mbunge huyo Nicholas Opiyo alirusha video katika ukurasa wake wa Twitter, ikimuonyesha Bobi Wine katika kiti cha magurudumu akiwasalimu wafuasi wake.
Kyagulanyi ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2017, amekuwa chachu miongoni mwa vijana ambapo mchambuzi wa masuala kisiasa nchini Uganda Rosebell Kagumire amesema Bobi Wine hakika ni mwiba na anampa changamoto rais Museveni mwenye umri wa miaka 74 changamoto ambayo hakuwahi kukabiliana nayo katika utawala wake wa miaka 32.
Rais Museveni, ambaye aliingia madarakani tangu mwaka1986, anatarajiwa kurefusha muda wake ifikapo mwaka 2021 baada ya mabadiliko ya katiba kupitishwa mwaka jana ili kufuta kipengee cha umri wa rais wa nchi hiyo. Kizazi cha vijana kinahofia kwamba rais Museveni aliyezeeka ana nia ya kutawala maisha baada ya kuwa madarakani kwa miaka 32 hadi sasa.
Bobi Wine pamoja na wabunge wengine kadhaa walishitakiwa wiki iliyopita baada ya waandamanaji kupiga mawe gari la rais Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi. Kukamatwa kwake kumesababisha watu kufanya maandamano na vurugu nchini Uganda huku jamii ya kimataifa ikilaani mateso aliyopewa mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwanasiasa.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE
Mhariri:Sylvia Mwehozi