Hatimaye Meli yenye nafaka yaelekea Lebanon
3 Agosti 2022Timu ya pamoja ya uratibu yenye kujumuisha wawakilishi kutoka Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba meli hiyo haijabeba mizigo mingine ambayo haikuidhinishwa kama vile silaha.
Katika taarifa yake, Umoja wa Mataifa umesema kuwa timu hiyo imetumia takribani saa tatu kukagua mizigo na wafanyakazi wa meli ya Razoni ambayo ina bendera ya Sierra-Leone, iliyoondoka bandari ya Odessa siku ya Jumatatu ikiwa na shehena ya mahindi kutoka Ukraine.
Kwa upande wake, Ukraine imesema meli nyingine 17 tayari "zimepakia na zinasubiri kibali cha kuondoka" lakini bado hapajakuwa na taarifa juu ya lini zitaanza safari. Ingawa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameitaja safari ya meli ya Razoni, "kama hatua muhimu" lakini hakuna meli nyingine iliyoondoka Ukraine ndani ya saa 48 na maafisa kutoka pande zote hawakutoa sababu za kucheleweshwa.
Nchini Ukraine kwenyewe, taarifa za kijasusi za wizara a ulinzi ya Uingereza zimedokeza kwamba mashambulizi ya kushutukiza ya Ukraine katika mkoa wa Kusini mashariki wa Kherson yamezidisha matatizo kwa upande wa Urusi. Uingereza inadai kuwa shambulio la Ukraine dhidi ya treni ya kijeshi ya Urusi limevuruga kwa muda njia ya usambazaji kutokea rasi ya Crimea. Daraja la Antonivka ambalo liliharibiwa na makombora ya Ukraine, limefanya vigumu kwa Moscow kufanya usambazaji kwa jeshi lake linalokalia eneo la magharibi la mto Dnipro.Vikosi vya Ukraine vyakomboa makaazi 40 ya Kherson
Kwingineko, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ameashiria uwezekano wa kuendelea kufanya kazi kwa vinu vya nyukilia vilivyosalia wakati akiishutumu Urusi kwa kuzuia kupeleka mtambo muhimu unaosaidia kusafirisha gesi katika mataifa ya Ulaya. Scholz amesema kuongeza muda wa kufanya kazi kwa vinu vitatu vya nyukilia vilivyobaki Ujerumani "kunaweza kuleta maana."
"Kilicho muhimu kwangu ni kuweka wazi kuwa mtambo huu unaweza kutumwa wakati wowote na unaweza kutumika. Hakuna kitu kinachozuia kusafirishwa kwake kwenda Urusi, isipokuwa wanunuzi wa Urusi wanapaswa kutoa ishara kuwa pia wanataka mtambo na kutoa taarifa muhimu kwa ajili ya forodha, usafiri wa Urusi. Vibali vingine vyote vimepatikana."
Hata hivyo, Ikulu ya Urusi Kremlin imesema shirika la Gazprom linakosa nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kuufunga tena mtambo huo kwenye bomba la Nord Stream 1 linalosafirisha gesi kwenda Ujerumani.
Ujerumani imekuwa ikihangaika kutafuta vyanzo vya nishati ili kuzipa pengo liliotokana na kupunguzwa kwa kiwango cha usambazaji wa gesi kutoka Moscow.