Hatma ya makubaliano ya Brexit kujulikana mwezi Januari
11 Desemba 2018Msemaji wa May amewaeleza waandishi habari kwamba anatafuta njia ya kusuluhisha mgogoro uliopo kuhusu mpango wake haraka iwezekanavyo, na anapania kupata hakikisho analohitaji kutoka kwa viongozi wa Ulaya kabla ya Januari 21.
Alipoulizwa iwapo kutakuwepo na kura kabla ya siku hiyo, msemaji huyo alikubali, na kusema serikali itahakikisha suala hilo linawasilishwa bungeni kabla ya tarehe 21. Vile vile amesema May alikuwa na mkutano wa kufana mapema leo na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte, ambao ulikuwa mkutano wake wa kwanza wa kukutana na viongozi wa Ulaya. Viongou hao wawili waliafikiana kufanya kazi pamoja kupata suluhu ya hali ya sasa.
Wakati huo huo msemaji huyo amesema waziri mkuu May alitaja masuala tete ambayo yanashikiliwa na wengi kuhusu mpango wake. Aidha anasema alijadili haja ya kuwepo kwa mahakikisho zaidi juu ya hatua hiyo ili mpango wake na Umoja wa Ulaya upitishwe katika bunge la Uingereza.
Hayo yakijiri waziri wa ngazi ya chini wa Brexit Robin Walker amesema bunge litajadili na kupiga kura kwa hatua ambazo serikali itachukua iwapo Bi. May ana mpango wa kuuidhinisha. "Kwa kuzingatia nia iliyo wazi ya sheria ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ya mwaka 2018, serikali itahakikisha kwamba swali la iwapo tutakubali makubaliano, litalerejeshwa katika bunge kabla ya tarehe 21 Januari mwaka ujao,"amesema Walker.
Walker ameyasema hayo kufuatia swali la dharura aliloulizwa na mbunge mpinzani, ambaye alisema kuna mkanganyiko kufuatia iwapo serikali inaweza kuipuuza bunge na kujiondoa katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano iwapo ingetaka kufanya hivyo.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE
Mhariri: Josephat Charo